Clinton afanya mazungumzo na Singh | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 20.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Clinton afanya mazungumzo na Singh

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh, wazungumzia kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili.

default

Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh (kulia), akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton mjini New Delhi, India.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, leo ameanza mazungumzo na Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh, na maafisa wa ngazi wa juu kwa lengo la kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa pande hizo mbili pamoja na kukamilisha mapatano ya sehemu muhimu, kama vile ulinzi na nishati.

Ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini India tangu ashike wadhifa huo mwezi Januari, mwaka huu, Bibi Clinton na Bwana Singh wamejadiliana masuala kadhaa muhimu, ikiwemo ushirikiano wa India na Marekani na namna ya kukabiliana na changamoto za dunia. Katika mazungumzo hayo, India inatarajiwa kutangaza mapendekezo ya maeneo ya mradi wa Marekani wa ujenzi wa viwanda viwili vya kutengeneza nishati ya nyuklia utakaogharimu mabilioni ya dola. Awali, Robert Blake, Naibu Waziri wa masuala ya Kusini mwa Asia, alisema kuwa mpango huo ni neema kubwa kwa kampuni za Marekani.

Bibi Clinton amesema Rais Barack Obama wa Marekani anataka kuendeleza juhudi zilizoanzishwa na utawala wa mtangulizi wake, George Bush, za kuimarisha mazungumzo yanayoonyesha muelekeo muhimu wa India katika kukabiliana na masuala mbalimbali, kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, kuimarisha biashara na kudhibiti silaha za nyuklia na silaha nyingine.

Suala jingine muhimu ambalo Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani amelizungumzia ni kuhusu uhusiano wa India na Pakistan na ushirikiano wa makundi ya kigaidi, kama vile Al-Qaeda na Taliban yanavyotishia dunia.

Baada ya mazungumzo na waziri mkuu wa India, Bibi Clinton atakutana na Lal Krishna Advani, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini India cha Bharatiya Janata, na kisha atafanya mazungumzo na Sonia Ghandi, mwenyekiti wa Chama cha Congress.

Aidha, leo jioni Bibi Clinton anatarajia kukutana na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa India, SM Krishna, ambapo watajadili uimarishwaji wa masuala ya uchumi na kijeshi pamoja na kuziangazia sekta za elimu, kilimo, nishati na sayansi.

Mwezi Oktoba, mwaka uliopita, Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Condoleezza Rice, na waziri mwenzake wa India, Pranab Mukhrjee, walisaini mkataba wa kufungua mauzo ya teknolojia ya nyuklia ya kiraia nchini India kwa mara ya kwanza katika miongo mitatu. Mpango huo utaiwezesha India kupata teknolojia ya Marekani na nishati ya nyuklia kwa bei ya chini, ambapo India itauruhusu Umoja wa Mataifa kufanya ukaguzi wa vifaa vyake vya nishati ya nyuklia, lakini siyo katika maeneo ya kijeshi ambako nishati ya nyuklia inatengenezwa.

Katika kuonyesha umoja na mshikamano, Bibi Clinton amefikia katika hoteli ya Taj iliyoko mjini Mumbai, miongoni mwa hoteli zilizoshambuliwa na mabomu mwaka uliopita na kusababisha vifo vya watu 166.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/DPAE)

Mhariri: Miraji Othman


 • Tarehe 20.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IszB
 • Tarehe 20.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IszB
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com