City mabingwa Ngao ya Jamii | Michezo | DW | 06.08.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

City mabingwa Ngao ya Jamii

Manchester City waliendeleza pale walipoachia msimu uliopita kwa kuilaza Chelsea magoli mawili bila jawabu na kuibeba ngao ya jamii ambayo kawaida ndiyo inayofungua msimu wa ligi kuu ya England.

Sergio Aguero ndiye aliyewaangamiza The Blues kwa mabao yake mawili, moja mnamo kipindi cha kwanza na jingine baada ya mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa uwanjani Wembley. Wachambuzi wanaipa Manchester City nafasi ya kulitetea taji lake la ligi kuu ya England ila itakumbukwa kwamba timu ya mwisho kushinda ngao ya jamii na kusonga mbele na kushinda taji la ligi kuu nchini humo ilikuwa Manchester United katika msimu wa mwaka 2010-2011.

City walilishinda taji hilo bila wachezaji wao muhimu Kevin de Bruyne na Raheem Sterling ila kocha wao Pep Guardiola amethibitisha kwamba watapatikana kwa mechi yao ya kufungua msimu. Kocha huyo pia amemsifu mwenzake wa Chelsea Maurissio Sarri licha ya kumbwaga kwenye mechi ya Jumapili.

"Kwanza kabisa nina furaha kwamba kocha wa kiwango kama hiki yuko hapa kwenye ligi kuu. Nitajifunza mengi kwa kumuona kila wikendi, msimu uliopita ulikuwa mgumu hasa tulipocheza nao. Na sasa yuko hapa kwa hiyo nitajifunza mengi kuhusu mbinu zake hapa England," alisema Guardiola.

UEFA Championsleague | Manchester City v FC Basel (Reuters/J. Cairnduff)

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola

Chelsea lakini wanakabiliwa na kitisho cha kumpoteza mlinda lango wao nambari moja Thibaut Courtois ambaye amehusishwa na kuhamia Rreal Madrid. Lakini kocha wake Maurissio Sarri amesema anataraji kuwa mbelgiji huyo atasalia Stamford Bridge.

"Sijui. Kwa sasa Courtois ni mlinda lango wa klabu ya Chelsea. Sijui katika siku za usoni, inategemea na klabu lakini nafikiri inategemea na yeye mwenyewe zaidi.Lakini natumai Courtois atakuwa mlinda lango wetu," alisema Sarri.

Kwengineko Bayern Munich waliwalaza Manchester United goli moja kwa bila katika mechi ya kirafiki iliyochezwa katika uwanja wa Allianz Arena. Goli la Bayern lilifungwa katika dakika ya 59 ya mechi na kiungo mkabaji wa Uhispania Javi Martinez.

Kocha wa United Jose Mourinho baada ya mechi hiyo alisema huenda asiwe na kikosi anachokitaka watakapofungua kampeni yao ya kuwania ubingwa wa England siku ya Ijumaa ambapo watacheza na Leicester City.

Mwandishi: Jacob SafariReuters/AFP/DPA

Mhariri: Gakuba Daniel