1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CIA yajitetea kuhusu mateso ya watuhumiwa

Mohammed Khelef12 Desemba 2014

Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), John Brennan, amelitetea shirika lake dhidi ya tuhuma za Baraza la Seneti kwamba wamekuwa wakitumia mateso ya kikatili kuwahoji watuhumiwa wa ugaidi.

https://p.dw.com/p/1E35k
Mkurugenzi wa CIA, John Brennan.
Mkurugenzi wa CIA, John Brennan.Picha: Getty Images/AFP/J. Watson

Katika hali isiyo ya kawaida, jioni ya jana CIA iliamua kuvunja ukimya juu ya ripoti ya Baraza la Seneti iliyoonesha kuwa maafisa wa shirika hilo la kijasusi wamekuwa wakitumia mbinu zilizopigwa marufuku kisheria na pia kulidanganya bunge na taifa kuhusiana na operesheni zake za kusaka taarifa dhidi ya ugaidi.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CIA, mjini Virginia, Brennan alisema programu ya shirika hilo kuwahoji washukiwa iliisaidia sana Marekani kama baadhi ya maafisa wake walitumia njia alizoziita "za kuchukiza sana" ambazo "haifahamiki" ikiwa ziliwezesha kupatikana taarifa za maana.

"Tayari nimeshaeleza kwamba uhakiki wetu unaonesha kwamba programu ya kuwaweka kizuizini na kuwahoji washukiwa ilitoa taarifa zenye maana sana ambazo ziliisaidia Marekani kupangua mipango ya mashambulizi, kuwanasa magaidi na kuokoa maisha. Lakini nifahamike wazi, hatujasema kwamba ni matumizi ya mbinu hizo kali za kuhoji ndani ya programu hiyo ndizo zilizotuwezesha kupata taarifa hizo kutoka kwa mahabusu," alisema Brennan.

Washirika wa Marekani wangiwa na wasiwasi

Juzi, Baraza la Seneti lilitoa ripoti yake inayoonesha kwamba CIA iliipotosha Ikulu na umma wa Marekani kuhusu ilivyowatesa mahabusu baada ya mashambulizi ya tarehe 11 Septemba 2001, na ilitumia mbinu za kikatili na kinyama zaidi kuliko ilivyosema. Brennan amekiri baadhi ya maafisa wake walichupa mipaka katika mbinu zao za kuwahoji mahabusu.

Seneta Dianne Feinstein wa Kamati ya Uchunguzi iliyotoa Ripoti ya Folter.
Seneta Dianne Feinstein wa Kamati ya Uchunguzi iliyotoa Ripoti ya Folter.Picha: Reuters/Yuri Gripas

Washirikia wengi wa Marekani ambao walichangiana taarifa na CIA, sasa wameonesha wasiwasi, baada ya kuchapishwa kwa ripoti hiyo. Poland, Afghanistan, Uingereza na Saudi Arabia, ni miongoni mwa mataifa yanayoshirikiana na Marekani katika kile kinachoitwa "vita dhidi ya ugaidi" na ambayo viongozi wake wamejitokeza kuilaumu CIA baada ya ripoti hiyo.

"Bush alidanganya kuhusu Iraq"

Wakati hayo yakiendelea, CIA imechapisha barua inayoonesha kwamba walikuwa na mashaka na hoja ya rais wa zamani, George Bush, kuhalalisha vita vyake nchini Iraq.

Kuelekea uvamizi wa Machi 2003, makamu wa rais wa wakati huo, Dick Cheney, na wenziwe serikalini walisema mmoja wa watekaji nyara wa ndege zilizotumika kwenye mashambulizi ya Septemba 11, Mohammed Atta, alikuwa amekutana na jasusi wa Iraq, Ahmad al-Ani, mjini Prague, lakini barua hiyo iliyopelekwa kwa Seneta Carl Levin mwezi Machi mwaka huu, inaonesha kwamba hilo halikuwa kweli.

Levin anasema ameiruhusu CIA kuichapisha barua hiyo ili kuonesha namna Bush alivyoidanganya Marekani kabla ya uvamizi wa Iraq.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman