1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa za kizalendo ni kitisho kwa uhuru wa vyombo vya habari

Sylvia Mwehozi
25 Aprili 2018

Ripoti iliyotolewa na shirika la maripota wasio na mipaka RSF, inaonyesha kuwa kushamiri kwa siasa za kizalendo barani Ulaya, kumedhoofisha uhuru wa vyombo vya habari katika ukanda huo,ambako awali ilikuwa salama zaidi.

https://p.dw.com/p/2wcLO
Berlin Tag der Pressefreiheit
Picha: Imago/IPON

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la maripota wasio na mipaka RSF ya 2018 kuhusu faharasi ya uhuru wa vyombo vya habari, uhasama dhidi ya waandishi na vyombo vya habari ni kitisho kikubwa kwa demokrasia duniani kote, ikiwemo Ulaya. Ulaya ni ukanda ambao uhuru wa vyombo vya habari upo juu, lakini pia ulizidi kuwa mbaya kwa maeneo mengine kwa mwaka huu.

Kati ya nchi tano za juu ambako hali ya uhuru wa vyombo vya habari imeshuka zaidi, nne kati ya hizo ziko barani Ulaya. Malta, Slovakia, Jamhuri ya Czech na Serbia, kwa kiasi kikubwa zote zimeangukia katika viwango hivyo. Shirika hilo limeonyesha wasiwasi hasa kuhusu mauaji ya mwandishi Daphne Caruana Galizia wa Malta, yaliyofuatiwa na mauaji ya mwandishi mwingine wa habari za uchunguzi Jan Kuciak miezi mitano baadae.

Berlin Mahnwache Daphne Caruana Galizia Malta Journalistin
Mwandishi wa habari wa Malta, Daphne Caruana Galizia aliyeuawaPicha: Imago/C. Mang

Kutokana na kushamiri kwa siasa za kizalendo na viongozi "wababe" Ulaya itaendelea kushuka viwango, limesema shirika hilo. Christian Mihr ambaye ni mkuu wa shirika hilo la RSF tawi la Ujerumani ameieleza DW kuwa "nafikiri maendeleo katika Ulaya ya kati na mashariki yanaonyesha wazi kwamba tunashughulikia kesi nyingi ambako demokrasia haijaanzishwa, ambao uanachama wake ndani ya Umoja wa Ulaya unaweza kutokea mapema."

Kitisho cha Trump, China na Urusi

RSF imesema kwamba chuki dhidi ya waadishi wa habari "si tu katika utawala wa Uturuki na Misri" bali pia imeingia maeneo mengine. Shirika hilo linamtuhumu rais wa Marekani Donald Trump, Urusi na China kwa kuendelea kupambana na vyombo vya habari na kutafuta kikamilifu kukabiliana na uhuru wake .

Symbolbild Pressefreiheit
Wanaharakati wa RSF wakiwa wamejifunga kamba kuashiria waandishi wa habari waliofungwa jelaPicha: picture-alliance/dpa

Pia ripoti hiyo imeonesha wasiwasi juu ya "udhibiti na ufuatiliaji" wa waandishi wa habari nchini China pamoja na juhudi za rais Xi Jinping za kuuza nje mfano wake wa udhibiti wa vyombo vya habari katika maeneo ya bara la Asia. Ripoti hiyo inasema "Xi Jinping wa China anakaribia kuwa toleo la kisasa la utawala wa kiimla".

Nchi zinazoongoza kwa uhuru wa vyombo vya habari

Norway imeendelea kushikilia nafasi ya juu katika faharasi ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa mwaka wa pili mfululizo, wakati Korea Kaskazini ikisalia katika nafasi ya mwisho kati ya nchi 180 zilizopimwa viwango hivyo.

Nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika orodha hiyo ni Gambia, iliopanda kwa nafasi 22 hadi kufikia nafasi ya 122. Ujerumani imepanda nafasi moja hadi nafasi ya 15 wakati Marekani ikiangukia kwa nafasi 2 hadi kufikia nafasi ya 45.

Uturuki, ambayo imefunga idadi kubwa ya waandishi wa habari ulimwenguni kote, sasa ni miongoni mwa nchi 25 zenye ukandamizaji zaidi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dw

Mhariri: Iddi Ssessanga