China yakasirishwa na tuhuma za UN dhidi yake juu ya Darfur | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

China yakasirishwa na tuhuma za UN dhidi yake juu ya Darfur

China imeikataa ripoti iliyotolewa jana na jopo la timu ya wataalamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inayosema kuwa silaha za nchi hiyo zilitumika kuwashambulia walinda amani jimbo la Darfur, nchini Sudan.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan (kushoto) na Rais wa China Hu Jintao wakikagua gwaride la heshima wakati Rais Hu alipowasili Sudana mwaka 2007

Rais Omar al-Bashir wa Sudan (kushoto) na Rais wa China Hu Jintao wakikagua gwaride la heshima wakati Rais Hu alipowasili Sudana mwaka 2007

Leo (21 Oktoba 2010), China imeikataa ripoti iliyotolewa jana na jopo la timu ya wataalamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo inasema kwamba silaha za nchi hiyo zilitumika kuwashambulia walinda amani wa Umoja huo na Umoja wa Afrika katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya China, Ma Zhaoxu amewaambia waandishi wa habari leo hii jijini Beijing kwamba, nchi yake inaichukulia ripoti hiyo kama uzushi, kwani imejikita kwenye taarifa zisizo na uhakika.

Ma amesema kwamba, daima China imekuwa ikitekeleza kikamilifu na kwa umakini mkubwa, maazimio yote ya vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Sudan; na kwamba ni jambo lisilofaa kwa jopo husika kuweka tuhuma kama hizi dhidi ya nchi mwanachama kwenye ripoti yake ya kila mwaka.

Watoto wa Kisudan wakiwa wamesimama na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID

Watoto wa Kisudan wakiwa wamesimama na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID

Mwanadiplomasia mmoja jijini New York alinukuliwa na gazeti la Washington Post wiki iliyopita akisema kwamba, tuhuma hizi ni jambo zito sana kwa China na kwamba nchi hiyo haitaki ripoti hii ichapishwe. Lakini wakati Ma alipoulizwa ikiwa ni kweli nchi yake imejaribu kuzuia uchapishwaji wa ripoti hiyo, hakutaka kuthibitisha wala kukanusha, ila aliwashauri wataalamu wa Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na umakini.

Kwenye ripoti yao, wataalamu hao wanasema kwamba, vikosi vya Sudan vilitumia zaidi ya darzeni moja ya aina tafauti za silaha za Kichina dhidi ya waasi wa Darfur kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ripoti hiyo pia inataja kugunduliwa kwa magamba ya risasi za Kichina, katika eneo ambalo yalifanyika mashambulizi kadhaa dhidi ya kikosi cha pamoja cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Mapema katikati ya mwezi huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kuhakiki kazi za jopo hili la wataalamu, na hatimaye likapiga kura kuongeza muda wake nchini Sudan hadi mwaka ujao. Lakini kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa kwa waandishi wa habari, China haikupiga kura hiyo, kwa sababu ya kuwa na mashaka na ripoti iliyowasilishwa na jopo hilo.

China ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama na, kwa hivyo, ina kura ya turufu ambayo inaweza kuitumia kuzuia azimio lolote ambalo inadhani halifai. Vile vile, serikali ya China ni mshirika mkubwa wa serikali ya Sudan, ambapo baina yao pana biashara ya kuuziana na kununuliana mafuta na silaha.

Chini ya vikwazo ilivyowekewa Sudan hapo mwaka 2005, ni halali kuizuia nchi hiyo silaha kwa sharti kwamba serikali ya Sudana nayo itoe hakikisho la silaha hizo kutoingizwa Darfur, jimbo ambalo lilianza kushuhudia uasi dhidi ya serikali kuanzia mwaka 2003. Umoja wa Mataifa unakisia kwamba, kwa uchache, watu 300,000 wameuawa tangu kuanza kwa uasi huo.

Hivi sasa maafisa wa Umoja wa Mataifa wanajtayarisha kusimamia kura mbili za maoni nchini Sudan katika mwezi wa Januari mwakani, ambapo katika kura moja Wasudani wa Kusini wataamua ikiwa waendelee kuwa sehemu ya Sudan au wajitenge; na katika kura nyengine, wakaazi wa jimbo la kati la Abyei wataamua ikiwa wawe sehemu ya Sudan ya Kusini ama ya Kaskazini.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFPE

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 21.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PkGU
 • Tarehe 21.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PkGU
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com