1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yafanya mazoezi makubwa ya kijeshi na Belarus

Daniel Gakuba
11 Julai 2024

China inafanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja na Belarus karibu na mpaka wa Poland ambayo ni mwanachama wa NATO. Luteka hizo za washirika hao wa Urusi, zimeelezwa kuwa zenye lengo la kupambana na ugaidi.

https://p.dw.com/p/4i9la
China | Belarus | Mawaziri wa Ulinzi Viktor Khrenin na Li Shangfu
Waziri wa Ulinzi Belarus Viktor Khrenin na mwenzake wa China Li ShangfuPicha: Belarusian Defence Ministry/REUTERS

Luteka hizo za Belarus na China zilizopachikwa jina la ''shambulizi la Kipanga'' zilianza Jumatatu wiki hii na zitaendelea hadi katikati mwa mwezi huu wa Julai.

Wizara ya mambo ya nje ya China kupitia msemaji wake Lin Jian, imesema mazoezi hayo ya kijeshi yanaheshimu sheria za kimataifa, na hayailengi nchi yoyote.

''Mafunzo haya ya kijeshi ya pamoja kati ya China na Belarus yanafanyika kulingana na mipango ya ushirikiano wa kila mwaka baina ya nchi hizo mbili, ambao ni ushirikiano wa kawaida baina ya mataifa." Alisema Jian.

Soma pia:Erdogan amwambia Xi anataka mahusiano ya Uturuki-China yaimarike

Alionegeza kwamba licha ya mazoezi hayo kufanyika ikiwa ni mpango wa kawaida, yamezingatia sheria ya kimataifa, na hakuna nchi yoyote ile inayolengwa.

Lakini Poland inatazama kwa wasiwasi luteka hizo zinazowashirikisha wanajeshi wa China jirani na mpaka wake. Wizara yake ya ulinzi imesema inatambua kitisho cha mazoezi hayo, na kuongeza kuwa jeshi la nchi hiyo liko tayari kukabiliana na hali yoyote ile inayoweza kujitokeza.

Wachambuzi: Luteka zinalenga kutuma ujumbe kwa NATO

Kutokana na uhusiano unaozidi kuharibika kati ya NATO kwa upande mmoja na China na Urusi kwa upande mwingine, wachambuzi wanaamini kuwa kwa mazoezi hayo, Beijing inataka kutuma ujumbe wa tahadhari kwa washirika wa NATO, na kwamba tarehe na mahali yanakofanyika havikuchaguliwa kwa kubahatisha tu.

NATO ni nini?

Mtaalamu wa kituo cha sera za kigeni na ulinzi cha Stimson cha mjini Washington, Kelly Grieco, anasema kwa mazoezi hayo China inatuma ujumbe wa kisiasa zaidi kuliko wa kijeshi.

Soma pia:Putin na Xi wahudhuria mkutano wa kilele wa SCO huko Astana

 Grieco amekumbusha kuwa tayari China ilifanya mazoezi ya kupambana na ugaidi nchini Belarus mara nne kati ya mwaka 2011 na 2018, na kwamba tangu wakati huo ilikuwa haijayapanga mengine.

"Lakini ukweli kwamba mara hii yanafanyika karibu na mpaka wa Poland, yanabeba ujumbe mzito zaidi, amesema mtaalamu huyo." Alisema.

Ni jambo la kawaida kwa mataifa kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi sambamba na matukio muhimu katika kambi nyingine ya kisiasa, anasema Alice Ekman, mtafiti mkuu wa masuala ya Asia katika taasisi ya masomo ya usalama ya Umoja wa Ulaya.

Wakati luteka hizi za China na Belarus zikifanyika sambamba na mkutano wa kilele mjini Washington, Aprili mwaka jana Urusi na China zilifanya mazoezi ya pamoja katika Bahari ya China Mashariki, kwenye mkesha wa mkutano wa pamoja baina ya Marekani na washirika wake wa mashariki ya mbali, Japan na Korea Kusini.