1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na vitega uchumi Zambia

23 Oktoba 2008
https://p.dw.com/p/FfVj

Zambia inajaribu kuvutia vitega uchumi kutoka China, ambayo ni mshirika mkubwa wa soko linalokuwa barani Afrika kibiashara, na kupuuzia wasiwasi wa nchi za Magharibi juu ya utendaji kazi mbovu na rekodi ya haki za binadamu na kuwakaribisha Wachina kwa mikono miwili.

Nchi hiyo fukara iliyoko kusini mwa Afrika ni mchimbaji mkubwa wa shaba katika bara hilo na hivi karibuni itaanza kuchimba mafuta karibu na mpaka wake na Angola. Ili kuivutia China, Zambia imetoa vivutio vya kodi na mambo mengine mazuri, ikiwemo vibali vya haraka vya kufanya kazi kwa wafanyakazi wa Kichina.

Kampuni za Kichina kwa upande wao zimeahidi kuwekeza dola milioni 900 katika utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na shaba katika eneo la uchumi lililowekwa kwa ajili yao, ambako wanapata msamaha wa kodi katika gawio na ushuru wa forodha kwenye mitaji yao.

Wachunguzi wa mambo wanasema China inainga Zambia na katika nchi nyingine za Afrika kwa sababu ya mikopo wanayotoa bila masharti ikilinganishwa na nchi za Magharibi na wawekezaji wake wanaoonekana kama wasemaji wa kisiasa

Kaimu rais wa Zambia, Rupiah Banda ameunga mkono kujihusisha kwa China katika uchumi wa nchi hiyo na hatua hiyo imefanya kubadilika kwa kiongozi mkuu wa upinzani Michael Sata, katika suala la China, ambaye pia ni mpinzani wake katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 30 mwezi huu.

Katika uchaguzi wa mwisho wa urais uliofanyika miaka miwili iliyiopita, ambapo Sata alishindwa dhidi ya rais aliyefariki mwaka huu, Levy Mwanawasa, alitaka kuzuiwa kwa wawekezaji wa Kichina kwa madai wanachukua kazi za Wazambia na wanawalipa ujira mdogo wafanyakazi wa Kizambia. Lakini hivi sasa ameahidi kufanya kazi na wawekezaji wa Kichina.

Akizungumza katika kampeni za uchaguzi, Sata alisema watu walimnukuu vibaya kuhusu China, kwani alisema anawakaribisha wawekezaji wa China, lakini hataruhusu wafanye kazi zinazoweza kufanywa na Wazambia wenyewe kama vile wapika chakula masokoni na badala yake wanahitaji ujuzi wa teknolojia yao na watoe ajira nzuri.

Zambia inayotegemea madini ya Shaba na Cobalt kwa zaidi ya asilia 65 ya mapatano ya serikali na taifa hilo kwa jumla ambalo linaangaliwa na wachambuzi kuwa lenye utajiri wa mali asili, lakini likiwa na miundo mbinu duni na hivyo kutarajia kwamba China inaweza kusaidia kuikwamua hali hiyo.

Katika kile ambacho hivi sasa ni hali ya kawaida barani Afrika msukumo wa China kupata madini, petroli na nafasi za kazi kwa ajili ya raia pamoja na maendeleo ya viwanda vyake inashirikiana na mipango ya Serikali ya Zambia ili kuinua uwezo wa maeneo ya nchi zinazoendelea.

Nchi hiyo imesema imepata ahadi ya vitega uchumi vya amoja kwa moja kutoka n´gambo katika miezi minane ya hadi kufikia Agosti mwaka huu, na sehemu kubwa ni kutoka China.

Baadhi ya wananchi wa Zambia wana wasiwasi juu ya malengo ya China, kutokana na mmiminiko mkubwa wa vitega uchumi vyake katika nchi kadhaa za Afrika.

Wachina wanajulikana kwa kutoa zawadi kwa maafisa wa serikali, anasema Said Chibamba Kanyama, mchumi anayefanyia kazi zake mjini Lusaka.

Katika nchi zenye mapigano kama vile Sudan au Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, China ameonekana kama shetani bora kuliko nchi za Magharibi kwa sababi kampuni za nchi za Magharibi haziwezi kwenda katika maeneo yenye migogoro kwa jili ya ujenzi kama vile barabara.