′China na Afrika zisihusiane kwa bidhaa nafuu tu′ | Matukio ya Afrika | DW | 06.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

'China na Afrika zisihusiane kwa bidhaa nafuu tu'

Waziri wa Biashara wa Afrika Kusini, Rob Davies, ataka biashara kati ya China na Afrika lazima iende mbele zaidi ya uingizwaji wa vitu vya bei nafuu barani Afrika

Rais wa Afrika ya Kusini, Jachob Zuma (kushoto) na wa China, Hu Jintao

Rais wa Afrika ya Kusini, Jachob Zuma (kushoto) na wa China, Hu Jintao

Waziri Rob Davies amesema ni muhimu kujenga soko la ndani na soko la walaji wa ndani pia iwapo Afrika inataka kusonga mbele.

Amesema nchi barani Afrika zinahitaji kuchukua nafasi na kuanza kuzalisha badala ya kutegemea soko la nje madini na soko linalotegemea bidhaa kutoka nje.

Mahusiano kati ya China na bara la Afrika yanahitaji kuondoka kutoka kusafirisha malighafi China na uingizwaji wa bidhaa za bei nafuu, na kuelekea kwenye mahusiano yatakayolinufaisha bara hilo kiviwanda zaidi.

Waziri Rob Davies amesema licha ya kuwa China imetoa nafasi nzuri kwa bara la Afrika, lakini uhusiano huo upo katika hatua ambayo bara la Afrika sasa lisikubali ongezeko la kiasi cha kile ambacho tayari kinacho. Lakini bara la Afrika liangalie jinsi ya mahusiano hayo na China yataanza kuchangia katika masuala muhimu zaidi barani Afrika.

Maliasili ya barala la Afrika, imekuwa yakinunuliwa upesi na China, kuchochea uchumi wake unaokuwa kwa kasi, na madini ni bidhaa kubwa inayonunuliwa na nchi hiyo, wakati bidhaa kubwa zinazotoka china kwenda Afrika ni vifaa vya umeme ua vya kiufundi.

Liu Guijin, mwakilishi wa Masuala ya Afrika katika wizara ya mambo ya nje ya China, amesema China sasa itawekeza zaidi na kuelekeza nguvu katika kujenga viwanda.

Liu Guijin amasema kwa mfumo uliopo sasa hivi wa bishara katika ya China na Afrika sio mzuri kwa mtizamo wao kwa sasa, akimaanisha uhusiano wa kibiashara baina ya bara la Afrika na Marekani, Umoja wa Ulaya na Japan.

Kuna umuhimu wa nchi zilizoendelea, China na nchi za Afrika kukaa pamoja na kupanua mfumo wa biashara na uchumi wa bara la Afrika.

Liu Guijin amesema pia, ni vyema nchi za Afrika kutumia vyema mapato yatokanayo na bidhaa ili kupanua mfumo wa uchumi wa nchi hizo.

Biashara kati ya China na bara la Afrika ulipanda haraka mwaka hadi mwaka hadi kufikia asilimia 4.3 na hasa katika miezi 11 ya mwaka 2010.

China imekuwa mbia mkubwa wa biashara na Afrika tangu mwaka 2009 na imemwaga fedha katika bara hilo, na licha ya kukoselewa kwa kuunga mkono serikali fidhuli kama Sudan, lakini imepongezwa kwa kuwezesha miundombinu ambayo inahitajika barani humo.

Martin Davies mtaalamu wa masuala ya ushauri wa Frontier Advisory, amesema mahitaji ya China ya raslimali ndio yaliyosababisha uchumi wa Afrika kukuwa kwa kasi na sio sera za uchumi wala mipango ya kiuchumi ya nchi za Afrika.

China ilitumia fedha nyingi katika miongo miwili iliyopita kuwekeza katika raslimali za kudumu hatua ambayo ilisababisha uchumi wa nchi hiyo kukua na kuimarisha mahusiano ya biashara na Afrika.

Martin Davies amesema mambo yakianza kupoa, basi uchumi wa China mwaka huu utashuka kwa asilimia kadhaa.

Amesema bara la Afrika lisileweshwe na ukuaji huo kwa sababu maamuzi yanayofanywa China hayatadumu milele.

Mwandishi: Rose Athumani
Mhariri: Josephat Charo