China: Miaka 20 tangu michafuko ya Tiananmen | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.06.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

China: Miaka 20 tangu michafuko ya Tiananmen

China: Miaka 20 tangu kukandamizwa vuguvugu la kidemokrasia

default

Watu waliojeruhiwa katika michafuko ya Tiananmen mjini Peking, China, Mei 4, mwaka 1989, wanapelekwa hospitali

Ni miaka 20 tangu kutokea kumwagika damu na kukandamizwa kwa nguvu lile vuguvugu la kidemokrasia mjini Peking, jambo lililopelekea wizani wa dunia ubadilike kwa manufaa ya Uchina. Na hata hivyo, chama cha kikoministi cha Uchina kinabidi kijielezee juu yayale yaliotokea miaka 20 ilopita.

Kweli, historia inaweza kutokuwa na haki hivyo? Mtu anaweza kufikia uamuzi huo pale mtu anapoiangalia China. Peking ilizama katika damu pale yalipotokea yale mabadiliko ya kisiasa ambayo miaka 20 nyuma kutoka sasa yaliikaba na kuikomboa Ulaya Mashariki. Na hata hivyo, watawala wa kiimla bado wanatawala huko China, tena kwa nguvu zaidi kuliko wakati wowote mwengine.

China ambayo hapo kabla ilikuwa nchi inayoendelea sasa imekuwa ina uzito mkubwa wa kiuchumi duniani. China imekuwa mkopeshaji mkubwa wa Marekani; kwa miaka imekuwa ikigharimia kujaza pengo la nakisi ya bajeti ya serekali ya Marekani. Peke yake katika mwezi wa Machi, China ilinunua dhamana za fedha za serekali ya Marekani kwa kiasi cha karibu dola bilioni 24. Nchi hiyo ya Asia imekuwa ya pili kama mshirika mkubwa wa kibiashara wa Umoja wa Ulaya. Na pia huko Afrika na Marekani ya Kusini ushawishi wa China unapanuka, kupitia biashara na uwekezaji.

Kumbukumbu ya mbinu za kisiasa kutoka vyama vya Christian Democratic na Christian Social Union iliopelekwa mbele ya bunge la Ujerumani ilionya tangu mwaka 2007 kwamba China isiokuwa ya kidemokrasia inaweza ikaja kutambulika kuwa ni mtindo mbadala wa maendeleo; nchi hiyo inaweza kuwa ni mfano mzuri kwa watawala wa kiimla kuutumia katika kuhalalisha vitendo yao.

Lakini yote hayo yanafungamana vipi na visa vya kutisha vilivotokea katika uwanja wa amani wa Tiananmen miaka 20 iliopita? Wizara ya mambo ya kigeni ya China ilitetea kwa mara nyingine tena kuuliwa kwa wanafunzi wasiokuwa na silaha katika uwanja huo, katikati ya Peking, ikiashiria maendeleoi ya kiuchumi yaliopatikana katika miongo iliopita. Uongozi wa China bado unapinga kutathminiwa upya lile vuguvugu la demokrasia, na mazungumzo yoyote juu ya jambo hilo hukandamizwa. Chama cha kikoministi kinayachukulia mafanikio ya kiuchumi yaliojionea nchi hiyo kuwa ni mali yake, lakini kinakataa kubeba dhamana ya ule ukurasa wa kiza wa historia yake; na kinakataa pekee kubeba dhamana ya wale waliokufa mjini Peking katika msimu wa kiangazi wa mwaka 1989. Pia chama hicho kinakataa kubeba dhamana ya kadiri ya watu milioni 20 waliokufa katika ile kampeni ya kuleta marekebisho ya kilimo katika nchi hiyo, iliopewa jina la "Kusonga Mbele kwa Kasi" mwanzoni mwa miaka ya sitini, na pia kwa wahanga wa mapinduzi ya kitamaduni na kampeni nyingine zilizouingiza umma wa watu.

Hiyo ndio maana chama cha kikoministi cha China kimepoteza kuaminiwa na wananchi. Ule ukimya kamili ulioonekana baada ya mauaji ulilinganishwa na thamani za neema zilizopatikana. Na hata kuingia ndani ya chama cha kikoministi hivi sasa zaidi kunasababishwa na mtu kutaka kuwa na uhakika katika kazi alio nayo na kidogo kutokana na sababu za kinadharia. Kubakia na misingi ya uadilifu ni jambo ambalo halitiliwa maanani hivi sasa huko China. Hatari ya kuchipuka utaifa wa kupindukia ni jambo ambalo haliwezi kufunikwa, na Jamhuri ya Umma wa Uchina sio tulivu hivyo kama inavoonekana juu juu. Siku baada ya siku kunafanyik ile inayoitwa maandamano yasiokuwa ya kisheria.

Kuna watu wenye mawazo ya kina ndani ya chama ambao wanatambuwa kwamba kwa ajili ya utulivu wake, China inahitaji marekebisho ya kisiasa, inahitaji demokrasia zaidi. Ni kwa njia hiyo ndipo mizozo inaweza kudhibitiwa na kutanzuliwa. Hayo ndio yalikuwa mawazo ya Zhao Ziyang, kiongozi mwanageuzi wa chama cha cha kikoministi, ambaye aliondoshwa madarakani kwa vile wenye vichwa ngumu katika kamati kuu ya kisiasa ya chama hicho hawajakubaliana na siasa zake. Nguvu za kidemokrasia katika China zinaweza kuungw amkono na Ulaya, pale nguvu hizo zitakapowakilisha thamani zao kwa njia ya kujiamini na pale nguvu hizo zitakapoungana. • Tarehe 03.06.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/I2y7
 • Tarehe 03.06.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/I2y7
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com