1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto ngumu zamkabili Medvedev siku 100 madarakani

Mohamed Dahman14 Agosti 2008

Rais Dmitry Medvedev wa Urusi leo anadhimisha siku 100 katika Ikulu ya Urusi akijaribu kuimarisha uongozi wake akikabiliwa na changamoto mbali mbali za kukanganya kuanzia vita na Georgia hadi wawekezaji wenye hofu.

https://p.dw.com/p/Ewzx
Rais Dmitry Medvedev wa Urusi.Picha: AP

Medvedev amerithi kutoka kwa mtangulizi wake na mtu aliemjenga Vladimir Putin urithi mgumu unaojumuisha kujiamini,nchi inayonawiri kiuchumi inayoandamwa na ulimbikizaji mkubwa wa madaraka katika Ikulu ya Urusi,utawala dhaifu wa sheria na rushwa iliokithiri.

Mwanasheria huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 42 hana uzeofu katika uongozi wa kisiasa na ana kipaji kidogo jambo lililopelekea kuenea kwa dhana kubwa kwamba atakuwa mshirika mdogo wa Putin ambaye hivi sasa ni waziri mkuu na bado ni mwanasiasa mashuhuri kabisa nchini Urusi.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kituo cha Levada katikati ya mwezi wa Julai umeonyesha ni asilimia 9 tu ya Warusi wanaamini kwamba Medvedev ndie anayeongoza nchi. Asilimia 47 wanafikiri kwamba wanatawala pamoja wakati asilimia 36 wanaamini Putin bado ndie mwenye kushika hatamu za uongozi.

Mzozo juu ya jimbo la Georgia linalotaka kujitenga la Osseti Kusini limetowa mtihani juu nani anayeshika hatamu hizo.

Urusi ilituma vikosi,ndege na meli za kivita wiki iliopita kuzima jaribio la Georgia kulichukuwa tena jimbo hilo na kuvirudisha nyuma vikosi vya Georgia.

Katika utawala wake wa siku za kwanza 100 Medvedev alivuruga matumaini kwamba yumkini akaonyesha msimamo laini katika malumabano kadhaa ya kidiplomasia kuanzia mpango wa nuklea wa iran hadi mipango ya Marekani kuweka mfumo wa makombora ya kujihami Ulaya ya kati.

Wakati ushirika wa Putin na Medvedev umefanyakazi vizuri katika sera ya kigeni kumejitokeza mgawiko katika masuala ya ndani ya nchi.

Medvedev ameingia madarakani kwa ahadi za kuanzisha utawala wa sheria na kufunguwa zaidi uchumi ambayo ni matumaini ya jumuiya ya biashara ya Urusi yenye kuchukia kujihusisha kunaokongezeka kwa Ikuku ya Urusi katika uchumi na kuongezeka kwa urasimu.

Mawazo hayo pamoja na mipango ya kuufanyia mageuzi mfumo wa sheria ili kuwapa Warusi mahakama za haki yamepata pigo kubwa mwezi uliopita wakati Putin aliposhambulia kampuni ya Urusi ya makaa ya mawe na chuma Mechel kwa sera zake za upangaji bei na kusababaihsa kushuka kwa hisa zake katika Soko la Hisa la New York.

Wawekezaji wenye hofu walianza kuondowa fedha taslimu kutoka Urusi na kuporomosha masoko yake ya hisa.

Medvedev anakabiliwa na mitihami muhimu katika wiki zinazokuja.

Mzozo mkali kati ya wamiliki wa pamoja wa Urusi na Uingereza kampni inayoshika nafasi ya tatu kwa ukubwa nchini humo ya TNK- BP na hatima ya mkuu wa zamani wa kampuni ya mafuta ya YUKO Mikhail Khodorkovsky alioko gerezani ambaye anastahiki kuachiliwa kwa msamaha mwezi huu utatowa vidokezo juu ya dhamira zake.

Wachambuzi wanasema hukumu bado iko wazi kuamauwa iwapo Medvedev ambaye hana kambi yake mwenyewe ya madaraka anaweza kuwa kiongozi halisi katika ulimwengi wa kisisia nchini Urusi uliohodhiwa na siloviki maafisa walio karibu na mashirika ya usalama na sheria ambao wanadhibiti nchi hiyo kupitia mahusiano binafsi yasio rasmi.