Champions League ; David Moyes aiota Bayern Munich | Michezo | DW | 31.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Champions League ; David Moyes aiota Bayern Munich

Viongozi wa ligi nchini Uingereza, Italia, na Ujerumani wapoteza points wakati Chelsea imekubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace, Juventus Turin yaambulia patupu.

Fußball Bundesliga - Der FC Bayern München ist Meister

Kikosi cha Bayern Munich

Mfululizo wa ushindi wa mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich katika michezo 19 mfululizo ulifikia kikomo mwishoni mwa juma hili baada ya kuambulia sare ya mabao 3-3 dhidi ya Hoffenheim. Bayern walikuwa na mabao 3-1 kabla ya nusu ya kwanza ya mchezo kumalizika, lakini kipindi cha pili Bayern walijilegeza kidogo na vijana wa Hoffenheim walitumia hali hiyo kurejesha mabao yote na kumaliza mchezo huo kwa kupata sare ambayo ilikuwa ni kama ushindi dhidi ya kikosi hicho kisichoshindika cha Bayern Munich msimu huu kama anavyothibitisha mlinda mlango wa Bayern siku hiyo Tom Starke.

Fußball Bundesliga 28. Spieltag: Bayern Muenchen - Hoffenheim

Wachezaji wa Bayern Munich

"Huenda tulifikiria vingine kidogo na hali yetu katika kipindi cha pili haikuwa kama tulivyopanga, kama ninavyosema, kwamba hatukucheza kwa uwezo wetu na kukamilisha ushindi ama hata kushinda kwa mabao 3-2. Haikuwa hivyo, lakini kwa kuwa hatukuweza kukamilisha wajibu wetu, tumeonesha , kwamba sisi ni binadamu tu wa kawaida."

Marco Reus alipachika mabao matatu na kuipatia Borussia Dortmund ushindi mgumu wa mabao 3-2 dhidi ya VFB Stuttgart timu ambayo inapapia majaliwa yake na kutapa kubakia katika daraja la kwanza. Timu hizo zilikwenda mapumzikoni wakati Stuttgart ikiongoza kwa mabao 2-1. Marco Reus anasema ilikuwa kibarua kigumu.

"Goli la pili lilituzindua kidogo. Ilikuwa muhimu, kwamba kabla ya kwenda mapumzikoni tumeweza kupata bao. Na namini, wakati wote mchezo huo ulipokuwa ukienda , pamoja na nafasi kadhaa tulizozipata tuliendelea kucheza vizuri. Kutokana na nafasi tulizozipata inathitisha wazi kuwa tulistahili kushinda. Schalke ilishinda jana , ilikuwa ni muhimu kwamba leo tushinde.

Fußball Bundesliga 28. Spieltag: Stuttgart - Dortmund Reus

Marco Reus

Kushindwa kwa Stuttgart na kutumbukia katika nafasi ya 16 katika msimamo wa ligi , ambapo sasa inachungulia tundu la kuingia katika ligi ya daraja la pili pamoja na Hamburg SC zikiwa zinatengana tu timu hizo kwa tofauti ya magoli zikiwa na polints 24 kila moja inaiweka timu hyo katika hali ya mashaka makubwa.

Ligi za Ulaya

Kwingineko barani Ulaya Liverpool imejisogeza hadi kileleni mwa Premier League kwa mara ya kwanza tangu mwezi wa desemba mwaka jana kwa ushindi wa kishondo wa mabao 4-0 dhidi ya Tottenham Hot Spurs wakati timu zote zinazoifukuzia zikiwa zimepoteza points. Chelsea ilipata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace,. wakati Arsenal ilitoka sare ya bao 1-1 na Manchester City na kuiacha Liverpool ikiwa points mbili juu ya msimamo wa ligi.

Deutschland Großbritannien Fußball Audi-Cup 2013 Manchester City gegen FC Bayern München

Wachezaji wa Manchester City

Huko Uhispania Atletico Madrid imepiga hatua kuelekea kuvishwa taji la msimu huu katika La Liga baada ya kupata ushindi wa mabao 2-2 dhidi ya Atletico Bilbao huku timu zote tatu za juu zikipokea ushindi siku ya Jumamosi.

Champions League

Champions League , duru ya robo fainali inafungua milango kesho Jumanne huko Old Trafford Manchester na Camp Nou mjini Barcelona.

Manchester United na Real Madrid zinakumbana na timu zilizoingia fainali ya Champions League msimu uliopita Bayern Munich na Borussia Dortmund wakati zikiwania kuokoa msimu ambao unaonekana kwenda kombo wa ligi za nchi zao kwa kuweka manbo sawa katika Champions League.

FC Everton Trainer David Moyes

David Moyes wa Manchester United

United inawakaribisha mabingwa watetezi Bayern Munich, ambao tayari wamekamilisha kazi ya kulitetea taji la ligi msimu wa 2014 katika mchezo wa kwanza wa robo fainali hapo kesho, wakati Real inatiana kifuani tena na Dortmund siku ya Jumatano katika uwanja wa Santiago Bernabeu.

Manchester United ndio wanyonge katika mchezo huo lakini kikosi cha kocha David Moyes kinaweza kujipiga kifua kutokana na ilivyofanya katika mchezo wa pili wa timu 16 bora dhidi ya Olympiakos Piräus pamoja na ushindi wa kwanza nyumbani katika Premier League tangu mwishoni mwa Januari kwa ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Aston Villa.

Real pia imerejea katika mbinu za ushindi kwa kuikandika Rayo Vallecano kwa mabao 5-0 mwishoni mwa juma.

Cristiano Ronaldo na kikosi chake kinawaza kulipiza kisasi dhidi ya borussia Dortmund. Hali hiyo inasaidiwa na kutokuwapo siku ya Jumatano kwa mshambuliaji hatari wa Dorttmund Robert Lewandowski ambaye amezuiwa kucheza kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Kesho(01.04.2014) Manchester United itakumbana na Bayern Munich na Barcelona itaumana na viongozi wa sasa wa La Liga Atletico Madrid.

Juventus Turin inayoongoza katika ligi ya Italia Serie A imepata pigo mwishoni mwa juma , wakati uongozi wake ulipopunguzwa hadi points 11 baada ya kupata kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya SSC Napoli.

Hapo mapema AS Roma iliyoko katika nafasi ya pili ilifanya kile kinachostahili kwa kushinda dhidi ya Sassuolo kwa mabao pia 2-0. Juventus ambayo inaelekea kupata ubingwa wake wa tatu mfululizo msimu huu ina points 81 kutokana na michezo 31 iliyocheza msimu huu na Roma wana points 70 wakiwa na mchezo mmoja zaidi.

Champions League barani Afrika

Huko Barani Afrika Zamalek ya Misri ilipitisha mipira mara tano katika nyavu za Nkana Red Devils ya Zambia na kujisafishia njia kuingia katika awamu ya makundi katika Champions League barani Afrika katika mchezo uliofanyika mwishoni mwa juma bila mashabiki mjini Cairo.

Timu zilizofanikiwa kuingia katika duru hiyo ni pamoja na ASEC Mimosas ya Cote D'Ivoire, Bayelsa Untd ya Nigeria, CA Bizertin ya Tunisia, Difaa El-Jadida ya Morocco , Djoliba ya Mali, Etoile sahel ya Tunisia, Medeama ya Ghana na Petro Atletico ya Angola.

Japan iko tayari kuwa wenyeji wa fainali za kombe la dunia iwapo shirikisho la kandanda duniani FIFA litaiondoa Qatar kuwa mwenyeji kuhusiana na madai ya rushwa. Rais wa shirikisho la kandanda la Japan JFA Kuniya daini amesema nchi hiyo ,ambayo mji wake mkuu Tokyo utakuwa mwenyeji wa mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2020 itajitolea kuchukua nafasi hiyo iwapo itajitokeza kuwa Qatar itaondolewa.

Nae kocha soka nchini Marekani Jurgen Klinsmann amemteua kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Berti Vogts kuwa mshauri maalum wa kikosi chake kwa ajili ya fainali za kombe la dunia zinazoaza Juni mwaka huu nchini Brazil. wataalamu hao wana uhusiano wa karibu, baada ya Vogts kuwa kocha wa kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani, ikiwa ni pamoja na Klinsmann ambacho kilitwaa ubingwa wa mataifa ya ulaya mwaka 1996 nchini Uingereza.

Mbio za magari.

Mercedes inawania kuchukua ubingwa mara tatu wakati mbio za magari za Formula One zitakapokwenda Bahrain mwishoni mwa juma lijalo baada ya kupata ushindi wao wa kwanza kati ya ushindi mara mbili katika enzi za sasa. Baada ya Luwis Hamilton kutamalaki katika mbio za Malaysia Grand Prix , akimshinda dereva mwenzake katika timu ya Mercedes Nico Rosberg, timu hiyo ya magari ya Ujerumani imeonesha kuwa inaweza kuipiku timu ya Red Bull, ya bingwa mtetezi Sebastian Vettel.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman