Champions League ; Bayern yaibuka kidedea | Michezo | DW | 20.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Champions League ; Bayern yaibuka kidedea

Mabingwa watetezi wa Champions League Bayern Munich walinusurika wimbi la mashambulio makubwa ya mapema kipindi cha kwanza na kufanikiwa kukiangusha kikosi cha watu 10 cha Arsenal London kwa mabao 2-0.

Arsenal FC vs Bayern Munich

Toni Kroos baada ya kupachika bao

Ni katika usiku wa mpambano wa vuta nikuvute jana usiku(19.02.2014) ambapo timu zote zilikosa mikwaju ya penalti na mlinda mlango wa timu ya wenyeji Wojciech Szczesny kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Yalikuwa magoli ya kipindi cha pili ya Toni Kroos na Thomas Mueller ambayo yaliwapa mabingwa hao watetezi ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya kikosi cha watu 10 cha Arsenal na kujikita karibu na kupata tikiti yao ya robo fainali.

Arsenal FC vs Bayern Munich

Refa akimuonesha mlinda mlango Szczesny kadi nyekundu

Wakosa penalti

Timu zote zilishindwa kupachika mabao kwa njia ya penalti, wakati mchezaji wa kiungo wa Arsenal Mesut Ozil alipoupiga mpira mikononi mwa mlinda mlango Manuel Neuer, na pia mchezaji wa kati wa Bayern David Alaba alipopiga mpira uliogonga mwamba wa goli.

Szczesny alitolewa nje katika dakika ya 37 kufuatia kumwangusha Arjen Robben.

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger alionesha kufadhaishwa dhahiri katika uamuzi wa kumtoa nje mlinda mlango Szczesny , akisema ulikuwa mchezo mzuri hadi nusu ya kwanza ya mchezo huo kumalizika.

Mesut Özil Arsenal London Fußball

Mesut Özil alikosa penalti

Uamuzi huo uliuua mchezo, Wenger amesema. Mchezo hadi wakati huo ulikuwa wa hali ya juu kabisa. Sehemu ya pili haikuwa na lolote. Ilikuwa ni mchezo wa upande mmoja.

Kocha wa Bayern Pep Guardiola anakanusha hilo lakini na anahisi kuwa ilikuwa ni penalti na ni sawa mlinda mlango huyo kutolewa nje. Guardiola anakiri hata hivyo , kuwa Arsenal walikuwa timu bora katika dakika 15 za mwanzo na kwamba kutolewa nje kwa mlinda mlango wao kumechangia kuisaidia timu yake.

Mchezo ulibadilika kabisa , kocha huyo wa zamani wa Barcelona amesema. Walikuwa na wachezaji tisa katika eneo la penalti na tulihitaji kuwa na subira.

Arsene Wenger

Kocha Arsene Wenger wa Arsenal

Majaaliwa ya Arsenal

Wakati majaliwa yanaielemea Arsenal London , kikosi hicho kutoka mjini London kinaweza kuwa na matumaini tu kuweza kurejea kile ilichokifanya mwaka jana na kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Bayern katika duru ya pili hapo Machi 11.

Katika mchezo mwingine usiku huo Atletico Madrid ya Uhispania ilifanikiwa kuishinda AC Milan ya Italia kwa bao 1-0 , bao lililowekwa wavuni na mshambuliaji wao Diego Costa.

Timu hiyo ambayo ni mwakilishi pekee wa ligi ya Italia Serie A katika kinyang'anyiro hicho katika awamu ya mtoano iliweza tu kupeleka mipira mara mbili na kugonga mlingoti wa goli kabla ya kukubali goli hilo lililofungwa na Diego Costa.

Tulicheza mchezo mzuri sana katika kipindi cha kwanza , tuligonga mlingoti wa goli mara mbili, tulitengeneza nafasi kadha na kisha, karibu na mwisho, wakafunga bao, nahodha wa Milan Kaka amewaambia waandishi habari.

Fußball Testspiele FC Bayern München gegen FC Barcelona

Kocha Pep Guardiola wa Bayern Munich

Michezo mingine itafanyika wiki ijayo Jumanne na Jumatano, wakati timu nyingine mbili za Ujerumani Borussia Dortmund na Schalke 04 zitakapoingia dimbani kupambana na Zenit St Petersburg na Schalke kupambana na Real Madrid.

Leo(20.02.2014) kutakuwa na michezo ya duru ya mtoano ya kombe la Europa League ambapo timu pekee ya Ujerumani Eintracht Frankfurt inashiriki.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre