Chama cha Sarkozy Chashinda Uchaguzi Mabaraza ya Wilaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Chama cha Sarkozy Chashinda Uchaguzi Mabaraza ya Wilaya

Uchaguzi wa mabaraza ya wilaya nchini Ufaransa umevipa ushindi mkubwa vyama vya mrengo wa kulia vinavyoongozwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Nicolas Sarkozy, na kukipa pigo chama tawala cha Francois Hollande.

Nicolas Sarkozy, rais wa Zamani wa Ufaransa ambaye chama chake kimepata ushindi wa chaguzi za mabaraza ya wilaya

Nicolas Sarkozy, rais wa Zamani wa Ufaransa ambaye chama chake kimepata ushindi wa chaguzi za mabaraza ya wilaya

Kulingana na matokeo yaliyochapishwa na shirika la habari la AFP, chama cha kihafidhina cha UMP cha aliyekuwa rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy pamoja na vyama vingine washirika vya mrengo wa kulia vimejishindia jumla ya viti 66 kati ya 101 vilivyokuwa vikiwaniwa.

Chama tawala cha kisoshalisti cha rais Francois Hollande kimeadhibiwa na wapiga kura kwa kushindwa kuufufua uchumi wa nchi, na kimeambulia viti 34 tu. Wakati matokeo hayo yalipochapishwa, kiti kimoja kilikuwa bado hakijapata mshindi.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande: Wafuasi wake wanahofia huenda ataangushwa katika uchaguzi wa mwaka 2017

Rais wa Ufaransa Francois Hollande: Wafuasi wake wanahofia huenda ataangushwa katika uchaguzi wa mwaka 2017

Kwa matokeo hayo, vyama vya mrengo wa kulia vimevinyakua viti 25 ambavyo vilikuwa vikishikiliwa na chama cha kisoshalisti, ambacho kimeweza kukichukua kiti kimoja tu kutoka kwa wapinzani wake.

Sarkozy azishambulia sera ya Hollande

Nicolas Sarkozy ameutumia ushindi wa chama chake kuzishambulia sera za rais Francois Hollande ambaye alichukua wadhifa huo baada ya kumwangusha Sarkozy katika uchaguzi uliopita.

''Kupitia kura zao, wafaransa wengi wamezikataa sera za rais Francois Hollande na serikali yake. Haijawahi kutokea kabla, kwa chama tawala kupoteza viti vingi kama ilivyotokea wakati huu. Haijawahi kutokea serikali iliyoko madarakani ikakataliwa kiasi hiki. Hakuna chama kilichiowahi kushindwa kiasi hiki katika ngazi zote''. Amesema Sarkozy.

Chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Front FN kinachoongozwa na Marine Le Pen, ambacho kilishinda robo ya viti katika duru ya kwanza ya uchaguzi huu, hakikutarajiwa kupata udhibiti wa baraza lolote la wilaya, sababu mojawapo ikiwa kwamba vyama vikubwa hushirikiana katika duru ya pili kukinyima ushindi.

Hata hivyo kimejishindia viti vingi katika mabaraza mbali mbali, kiasi cha kumfanya kiongozi wake Marine Le Pen kujitapa kwamba kwa sasa chama chao kimekuwa nguvu inayotambulika katika maeneo mengi ya nchi. ''Uchaguzi huu ni hatua muhimu kwa vuguvugu la kizalendo kuelekea madarakani'', amesema bi Le Pen.

Hofu katika kambi ya wasoshalisti

Chama cha kisoshalisti kilichopo madarakani kimeelezea hofu kwamba kushindwa kwake katika uchaguzi huu wa mabaraza ya wilaya ambayo yana madaraka kiasi katika masuala ya kijamii, huenda kukakiandama katika chaguzi za mikoa na za kitaifa zinazokuja.

Marine Le Pen: Ushindi huu ni hatua kuelekea Ikulu

Marine Le Pen: Ushindi huu ni hatua kuelekea Ikulu

Waziri Mkuu Manuel Valls amekiri kwamba kushindwa huko ni kipigo kwao, na kuongeza kuwa mafanikio kiliyoyapata chama cha FN ni makubwa mno.

Amesema wafaransa wametoa kauli yao, ambayo inadhihirisha hasira waliyo nayo kutokana na karaha za kila siku maishani. Kiongozi huyo ameahidi kwamba serikali itaongeza mara dufu juhudi za kuuboresha uchumi wa Ufaransa, ambao ni wa pili kwa ukubwa barani Ulaya.

Mshauri wa Rais Francois Hollande ambaye umaarufu wake umeporomoka miongoni mwa wapiga kura, ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba kila mmoja katika Ikulu yake anayo hofu kuwa ataondolewa katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com