1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Demokratik chaongoza katika matokeo ya awali

Zainab Aziz
7 Novemba 2018

Kura zimeanza kuhesabiwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani. Uchaguzi huu unazingatiwa kuwa kura ya maoni kwa rais Donald Trump.

https://p.dw.com/p/37mhb
USA Midterm-Wahlen 2018
Picha: Getty Images/AFP/A. Caballero-Reynolds

Wamarekani wamepiga kura muhimu ya katikati ya muhula ambayo ni mtihani wa kwanza kwa rais Donald Trump. Zoezi hilo ni kama kura ya maoni kwa utawala wake. Hadi sasa katika baadhi ya maeneo vituo vya kupigia kura vimeshafungwa na matokeo ya kwanza yameshajulikana. Mjumbe anayejitegemea Berney Sanders pia amechaguliwa tena kuwa seneta katika jimbo lake la Vermont.

Katika jimbo la Virginia mjumbe wa chama cha Demokratik Tim Kaine amechaguliwa tena kuwa seneta baada ya kumshinda mjumbe wa chama cha Republican Corey Stewert ambaye ni mshirika mkubwa wa rais Donald Trump. Ushindi wa Tim Kaine katika jimbo hilo la Virginia unazingatiwa kuwa muhimu sana katika juhudi za chama cha Demokratik za kulidhibiti tena baraza la wawakilishi.

Chama cha Demokratik kinahitahitaji kupata viti zaidi ya 23 katika bunge lenye viti 435 ili kuweza kulidhibiti baraza la wawakilishi ambalo hadi sasa linadhibitiwa na chama cha Republican.Mtaalamu mmoja wa masuala ya uchaguzi kutoka kwenye kituo cha siasa cha chuo kikuuu cha Virginia ametabiri kwamba chama cha demokratik kitapata viti visivyopungua 30 katikam baraza la wawakilishi.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/C. Barria

Mjumbe wa chama cha Republican Charlie Baker amechaguliwa kutumikia muhula wa pili kama gavana wa jimbo la Massachusetts baada ya kumshinda mjumbe wa chama cha Demokratik. Mjumbe wa chama cha Republican Mike Braun amechaguliwa kuwa seneta katika jimbo la Indiana.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la AP, takriban asilimia 40 ya wapiga kura wamempinga rais Trump. Uchunguzi huo unaonesha kuwa katika kila watu wanne mmoja amemuunga mkono rais huyo na pia umebainisha kwamba miongoni mwa wapiga kura 10 sita wamesema Marekani inaelekea kubaya chini ya uongozi wa rais Trump.

Wakati huo huo rais Donald Trump na mkewe Melania pamoja na marafiki na familia yao wanafuatilia matokeo ya uchaguzi kwenye ikulu. Ikiwa wajumbe wa chama cha Demokratik watalidhibiti baraza la seneti au baraza la wawakilishi wataweza kuikwamisha ajenda ya rais Trump kwa miaka miwili ijayo.

Katika uchaguzi huo wanawake wengi wameshiriki katika kinyang'anyiro cha kuwania viti. Wanawake 237 waligombea viti kwenye baraza la uwakilishi. Wanawake hao pia wamegombea ugavana katika majimbo 16 mnamo mwaka huu. Masuala muhimu yaliyozingatiwa katika katika uchaguzi huo yalikuwa juu ya bima ya afya na uhamiaji.

Mwanadishi: Zainab Aziz/AP/DPA

Mhariri: Sylvia Mwehozi