1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chakula cha msaada hatimaye chawasili Yemen

Caro Robi
27 Novemba 2017

Yemen imepokea shehena ya kwanza ya msaada wa chakula Jumapili. Meli iliyokuwa imebeba tani 5,500 ya unga iliwasili katika bandari ya Saleef ikiwa shehena ya kwanza ya msaada wa chakula kuwasili tangu tarehe 6 mwezi huu.

https://p.dw.com/p/2oJD0
Jemen Kind Unterernährung
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mohammed

Abeer Etefa, msemaji wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP katika kanda ya Mashariki ya kati na kaskazini mwa Afrika amesema tani 25,000 ya ngano zitapakuliwa leo kutoka meli iliyowasili magharibi mwa Yemen katika bandari ya Saleef, iliyoko kilomita 70 kutoka bandari kuu ya Hodeida.

Bandari ya Hodeida ndiyo inayotumika zaidi na mashirika ya Umoja wa Mataifa inayotoa misaada ya chakula na matibabu kwani ndiyo iliyo karibu zaidi kwa idadi kubwa ya raia wanaohitaji misaada ya dharura. Eneo hilo liko chini ya udhibiti wa waasi wa Houthi.

Mashirika ya kiutu yapewa ridhaa

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu imesema imepewa ridhaa ya ndege zake kurejea kusafiri kuelekea Sanaa lakini ikaongeza kuwa meli za kubeba vyakula na dawa kuelekea bandari ya Hodeida bado zinazuiwa.

Picha inayoonyesha bandari ya Hodeida iliyoko nchini Yemen
Bandari ya Hodeida nchini YemenPicha: Getty Images/AFP/A. Hyder

Hapo jana, meli moja ilitia nanga katika bandari hiyo, lakini WFP ilisema siyo ya mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa misaada na huenda ni meli ya kubeba mizigo. Naibu mkuu wa bandari hiyo Yahya Sharafeddine amethibitisha kuwa haikuwa imebeba misaada bali inamilikiwa na wafanyabiashara.

Mapema mwezi huu, Saudi Arabia ilisema ilichukua hatua ya kuweka vizuizi vya usafiri nchini Yemen ili kuzuia silaha kutoka Iran zilizokusudiwa kupewa waasi wa Houthi kuingizwa Yemen na kujibu hatua ya waasi ya kufyatua kombora karibu na uwanja wa ndege ulio katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh. Iran imekanusha madai kuwa inawapa silaha waasi wa Houthi.

Hatua ya kuzifunga njia za usafiri za majini, angani na ardhini Yemen ilishutumiwa vikali na jumuiya ya kimataifa kutokana na kwamba Wayemen milioni saba wanategemea chakula cha msaada kuishi.

Wayemen milioni saba wanategemea misaada

Siku ya Jumamosi, ndege nne zilizobeba misaada na wafanyakazi wa kutoa misaada ya kiutu ziliruhusiwa kutua katika uwanja wa ndege wa Sanaa. Shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limetuma chanjo kwa ajili ya watoto laki sita. Mkurugenzi wa UNICEF katika kanda hiyo Geert Cappelaere amesema wanatumai vizuizi vyote vitaondolewa ili waweze kuwafikia watu wengi wanaohitaji misaada.

Ndege iliyobeba misaada ya chakula na matibabu yawasili katika uwanja wa ndege wa Sanaa nchini Yemen
Misaada yawasili katika uwanja wa ndege wa SanaaPicha: Reuters

Vita vya Yemen vilivyoanza tangu 2015, vimewaua kiasi ya watu 8,600 na wengine 2,000 wamefariki dunia kutokana na kipindupindu.

Yemen inategemea pakubwa misaada ya chakula kuweza kulisha watu wake na mashirika ya kutoa misaada yameonya kuwa misaad ya kiutu inayotolewa haikidhii mahitaji yanayohitajika. Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watoto milioni 11 katika taifa hilo linalokumbwa na mzozo, wanahitaji kwa dharura misaada ya kibinadamu.

Huku hayo yakijiri, maafisa wa usalama nchini humo wamesema ndege ya kijeshi ya  Marekani isiyoendeshwa na rubani imewauwa wapiganaji watatu wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda katika jimbo la Bayda. Hilo ni shambulizi la tatu ndani ya kipindi cha wiki moja katika jimbo hilo ambalo ni ngome ya wanamgambo wa Al Qaeda.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo