1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema wazindua rasmi kampeni za uchaguzi mkuu

George Njogopa28 Agosti 2020

Vyama vya siasa nchini Tanzania vimeanza kuweka mguu sawa kuelekea katika uchaguzi mkuu huku chama cha demokrasia na maendeleo Chadema, kikiwa cha kwanza kuzindua kampeni zake.

https://p.dw.com/p/3hd9D
Tansania Wahlen | Treffen der Chadema-Delegierten in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

Chama cha Chadema kinaanzisha kampeni zake mchana huu katika viwanja vya Zakheem eneo la Mbagala na baadaye kuzunguka katika maeneo kadhaa ya jiji hilo.

Kwa lugha nyingine unaweza kusema kwamba sasa kumekucha wakati ambapo vyama vyote vimejiweka tayari kuanza kushambulia majukwa kwa hoja na vijembe vya hapa na pale vikijaribu kuwavutia wapiga kura kuelekea katika uchaguzi huo wa mwezi wa Oktoba.

Chadema ndiyo inayoanza kulifungua pazia la kampeni na wakati huu wanachama pamoja na wafuasi wake wameanza kumiminika katika viwanja vya Zakheem ambako mgombea wake wa urais, Tundu Lissu atakayeambatana na mgombea mwenza watakapojitokeza kwa mara ya kwanza mbele ya hadhara tangu kufunguliwa kwa dirisha la kampeni hapo Agosti 26.

Chama hicho ambacho kinafanya kampeni kwa kauli mbiu ya Peoples Power yaani Nguvu ya Umma, kimetenga muda wa siku tatu kuzunguka maaneo ya jiji la Dar es salaam kunadi sera zake na huenda masuala kama kubinywa kwa vyama vya upinzani kufanya siasa, kukosekana uhuru wa maoni pamoja kunusurika katika shambulizi baya kuwahi kushuhudiwa kwa mwanasiasa wake, ikawa ni baadhi ya mambo yatayohanikiza kampeni zake.

Wanachama wake ambao pia wanatambulika kwa jina la Makamanda wanamwona mgombea wao, Tundu Lissu kama ni mtu atakayeweza kukabiliana vilivyo na chama tawala CCM kinachojivunia utendaji wa serikali yake inayotajwa kuimarisha uwajibikaji serikali, kupambana na rushwa na kuinyanyua sekta ya miundombinu.

Wengi wafuasi wa chama hicho wanaona kwamba kampeni za mwaka huu huenda zikawa na ushindani mkali hasa kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyopo.

CCM imepanga kuzindua kampeni zake kesho katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma na tayari jiji hilo limeanza kupambwa na bendera za chama hicho huku wanachama na wafuasi wake wakianza kuwasili.

Vyama vingine navyo vimekuwa na mipango hiyo hiyo ya kuanzisha kampeni zake mwishoni mwa wiki. Mgombea wa chama kimojawapo kinachojinadi na sera ya kugawa ubwabwa bure kwa wananchi, Hashim Rungwe amepanga kuanzisha kampeni zake huko Musoma, lakini anasema yuko katika mshangao mkubwa baada ya wagombea wake kutiliwa ngumu kupewa fomu kwa madai chama chake hakitambuliki.

Vyama vyote hivyo vina muda wa siku 60 kuzungumza na wapiga kura, kabla ya duru hii haijafikia tamati hapo Oktoba 27, siku moja kabla ya siku ya upigaji kura.