Chad kutuma wanajeshi Cameroon kupambana na Boko Haram | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Chad kutuma wanajeshi Cameroon kupambana na Boko Haram

Rais wa Cameroon Paul Biya ametangaza kuwa Chad itatuma kikosi kikubwa cha wanajeshi nchini mwake kusaidia katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa kundi la Boko Haram

Tangazo hilo lililototolewa na Rais wa Cameroon Paul Biya halikufafanua ni wanajeshi wangapi hasa watatumwa kuelekea Cameroon lakini inakuja siku moja baada ya serikali ya Chad kusema itasaidia kikamilifu katika kupambana na Boko Haram kundi la waasi lenye ngome yake nchini Nigeria lakini limetanua uasi wake hadi nchi jirani ya Cameroon.

Biya ameiomba jumuiya ya kimataifa kutuma majeshi kuweza kukabiliana na kitisho cha waasi wa Boko Haram ambao wameyateka maeneo makubwa ya kaskazini mwa Nigeria na kutishia usalama wa nchi jirani zinazopakana na Nigeria.

Boko Haram imezidisha mashambulizi

Kundi la Boko Haram ambalo linapania kuunda taifa la kiislamu kaskazini mwa kanda hiyo ya Afrika, limezidisha mashambulizi kaskazini mwa Nigeria huku taifa hilo kubwa zaidi kiuchumi barani Afrika likijiandaa kufanya uchaguzi mkuu mnamo tarehe 14 mwezi ujao.

Picha za satalaiti zinaonyesha uharibu wa Boko Haram mjini Baiga

Picha za satalaiti zinaonyesha uharibu wa Boko Haram mjini Baiga

Kundi hilo pia limefanya mashambulizi kadhaa kaskazini mwa Cameroon na kusababisha serikali kuwatuma maelfu ya wanajeshi kulinda mipaka.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu magharibi mwa Afrika Mohammed Ibn Chambas hapo jana alizihimiza Nigeria,Cameroon,Chad na Niger kuweka kando tofauti zao na kukubaliana kuhusu kuundwa kwa kikosi maalumu cha kijeshi kitakachopambana na Boko Haram.

Hayo yanakuja huku jeshi la Nigeria likisema limewaua waasi 42 wa Boko Haram walipojaribu kuuteka mji wa Biu ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria siku ya Jumanne wiki hii. Miongoni mwa waasi hao waliouawa 15 ni raia wa Chad.

Mike Omeri ambaye ni mratibu wa kituo cha kitaifa cha kutoa taarifa cha Nigeria amesema waasi wengine watano walikamatwa walipojaribu kutoroka na kwamba watachakuliwa hatua za kisheria kwa kuhusika na uhalifu dhidi ya serikali.

Rais Goodluck Jonathan azuru Maiduguri

Wakati huo huo, Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan hapo jana aliutembelea mji wa Maiduguri ambao umeshambuliwa mara kwa mara na Boko Haram. Akiwa katika ziara hiyo, Rais Jonathan alisema serikali haijashindwa katika jukumu lake la kuwalinda raia.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan(Kati kati) akifanya kampeini

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan(Kati kati) akifanya kampeini

Ziara hiyo ya Jonathan inaonekana na wachambuzi kuwa jaribio lake la kuwashawishi wapiga kura kumchagua tena katika uchaguzi ujao.

Mwanahabari Mohammed Salihu aliyeko Maiduguri amesema wanigeria wamekuwa wakifa kila uchao katika majimbo matatu ya kaskazini mwa Nigeria kutokana na mashambulizi ya Boko Haram na Rais hakufanya ziara katika maeneo hayo hadi wakati huu wa kampeini.

Kiasi ya watu milioni moja na laki tano wameachwa bila makaazi kaskazini mwa Nigeria kutokana na mashambulizi ya Boko Haram na inahofiwa kuwa wengi wao hawataweza kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

Tume ya uchaguzi nchini Nigeria imesema iko mbioni kutoa kadi za kupigia kura kwa waathiriwa hao kabla ya uchaguzi ili waweze kushiriki katika zoezi hilo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com