CCM Zanzibar warejesha fomu, ACT wafungua pazia | Matukio ya Afrika | DW | 30.06.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

CCM Zanzibar warejesha fomu, ACT wafungua pazia

Zoezi la kutangaza nia kuwani nafasi ya urais Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, CCM limekamilika baada ya wanachama 32 kurejesha katika mchakato ulioshuhudia ushindani mkubwa ndani ya chama hicho.

Miongoni mwa waliojitokeza ni wanawake watano na wanaume 27, mwaka huu ukiweka historia kwa wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kupita chaguzi zote zilizopita, ambapo mara ya mwisho alijitokeza mwanamke mmoja tu na wanaume wanane.

Katibu wa oganazaisheni ya chama hicho kwa upande wa Zanzibar, Galos Nyimbo amesema zoezi hilo limekwedna kwa nidhamu kubwa.

Hussein Mwinyi

Dk. Hussein Mwinyi ni miongoni wagombea wa usoni kupitia CCM Zanzibar.

Katika mchakato huo wanawake waliojitokeza walipongezwa na baadhi ya wanaharakati wa wanawake ikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake kwa upande wa Zanzibar, TAMWA kwa kushiriki katika kuwania madaraka ya juu ya uongozi ili kufikia asilimia 50 kwa 50 ambayo sasa hivi inahimizwa katika nchi mbalimbali duniani.

Hata hivyo, mmoja wa wagombea aliyechukua fomu Hussein Ibrahim Makungu, ametangaza kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho hata kabla ya kuanza kwa mchujo siku ya Jumatano. Hivyo majina 31 ndiyo yatakayorejeshwa kwa ajili ya mchujo.

Kwa mujibu wa ratiba za chama hicho mgombea atakayepitishwa na chama atajulikana Julai 10 baada ya kupigiwa kura na kamati kuu ya CCM katika jiji la Dodoma.

Tansania ACT Wazalendo Partei

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza nia kuwani urais kwa tiketi ya chama chake.

Katika hatua nyengine Chama cha ACT Wazalendo kinafungua pazia la uchukuaji wa fomu za kuwania urais wa Zanzibar na nafasi nyengine za ubunge, uwakilishi na udiwani ambazo zitaanza kutolewa hapo kesho Julai mosi na tayari mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza nia ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo.

Wagombea wa vyama vingine waliojitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi kama hiyo ni Said Soud wa chama cha Wakulima, AAFP, Juma Ali Khatib wa Ada TADEA, pamoja na Ambar Haji Khamis wa NCCR Mageuzi.