1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CARLETONVILLE:Mgodi wa Elandsrand kufungwa kwa muda

4 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7IV

Waziri wa Madini na Nishati wa Afrika Kusini Buyelwa Sonjica ameagiza kufungwa kwa muda kwa mgodi wa Elandsrand ambako operesheni kubwa ya uokozi inaendelea.Mamia ya wachimba mgodi walinasa hapo jana katika mgodi huo pale bomba la maji lilipopasuka na kusababisha uharibifu mkubwa.Mgodi huo unatarajiwa kufungwa kwa kipindi cha kati ya majuma matatu hadi 6 ili uchunguzi ufanyike kujua chanzo halisi cha mkasa huo.Mgodi huo ulioko jimbo la Gauteng unamilikiwa na kampuni ya dhahabu ya Harmony iliyo mzalishaji wa 5 kwa ukubwa wa dhahabu ulimwenguni.Mamia ya wachimba mgodi bado wamenasa chini ya ardhi kwenye eneo lililo na kina cha maili moja tangu jana asubuhi baada ya bomba lililoanguka kusababisha umeme kukatika.

Wafanyikazi takriban 1700 waliokolewa mchana wa leo .Kulingana na waziri huyo wa Migodi na Nishati kampuni ya dhahabu ya Harmony haikuonyesha rekodi nzuri ya usalama na kuongeza kuwa endapo itapatikana kuwa ilikiuka kanuni za usalama wa wafanyikazi itashtakiwa.

Shirika la Kitaifa la Wachimba Migodi NUM linalaumu kampuni ya dhahabu ya Harmony kwa kuzembea ukarabati na kueleza kuwa njia nyengine ya kutokea mgodini haikuweza kutumika kwani ilijaa maji.Mashirika ya wachimba migodi yamekuwa yakilalamika kila mara kuhusu idadi kubwa ya ajali na vifo katika migodi nchini Afrika Kusini.Afrika Kusini ni mchimbaji na mzalishaji mkubwa wa dhahabu na madini ya platinum ulimwenguni.