1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAIRO: Rais wa Misri, Hosni Mubarak, afadhaishwa na ukanda wa video kuhusu kunyongwa Saddam Hussein.

5 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCd6

Rais Hosni Mubarak wa Misri amesema kitendo cha kupiga picha za video wakati akitiwa kitanzi rais wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, ni fedheha na kinaudhi na kwamba wataalamu wa masuala ya sheria walipinga kuendeshwa kesi ya Saddam Hussein kwenye taifa ambalo bado limevamiwa na majeshi ya kigeni.

Hosni Mubarak aliliambia gazeti moja la Israil kwamba uamuzi wa kumnyonga Saddam Hussein katika sikukuu ya Idd al-dha haukuwa mzuri.

Rais huyo amesema alikuwa amewasiliana na Rais George W Bush kwa njia ya barua akitaka kuahirishwa adhabu hiyo kwa kuwa haukuwa wakati mwafaka wa kuitekeleza.

Hosni Mubarak amesema si jukumu lake kuamua endapo Saddam Hussein alistahili kunyongwa au la, lakini jinsi shughuli hiyo ilivyotekelezwa ilikwenda kinyume na maoni ya watalaamu wa kimataifa kuhusu hali ya Iraq.

Rais Mubarak na Saddam Hussein walikuwa marafiki wakubwa katika miaka ya themanini lakini urafiki wao ukaingia dosari baada ya Iraq kuishambulia Kuwait mwaka wa alfu moja mia tisa na tisini.

Rais Hosni Mubarak alikuwa ameitahadharisha Marekani kuishambulia Iraq akihofia ghasia kuzuka.