1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAF kuridhia Kombe la Dunia kuwa kila baada ya miaka miwili

Bruce Amani
25 Novemba 2021

Nchi wanachama za Kiafrika zinatarajiwa kuunga mkono kwa kauli moja mipango ya kuandaliwa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili na pia kuunga mkono kuundwa mashindano maalum ya Super League.

https://p.dw.com/p/43T74
Fußball CaF | Patrice Motsepe und FIFA Präsident Gianni Infantino
Picha: BackpagePix/empics/picture alliance

Uungwaji mkono wa kuandaliwa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili badala ya mzunguko wa sasa wa miaka minne tayari umeelezewa na rais wa CAF Patrice Motsepe na baraza hilo ambalo aghalabu huwa linaheshimu maamuzi linatarajiwa kuidhinisha mipango hiyo ya rais wa FIFA Gianni Infantino.

"Mojawapo ya wanufaika wakubwa wa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili ni nchi zinazoendelea,” alisema Motsepe katika kikao cha waandishi wa habari mwezi uliopita, na kwa mujibu wa duru za ndani, ataendeleza hoja kuwa mapato Zaidi ya Kombe la Dunia yatatiririka kwa wanachama wa Kiafrika na kuzipiga jeki hazina zao.

Haya yanakuja licha ya kitisho kwa tamasha maarufu la barani humo – Kombe la Mataifa ya Dunia. Huandaliwa kila baada ya miaka miwili, kwa sababu lilikuwa likileta asilimia 80 ya mapato ya CAF kabla ya shirikisho hilo kuanza kupewa ruzuku za kifedha kutoka FIFA.

Motsepe amekuwa mshirika wa karibu wa Infantino, ambaye ameshinikiza vikali katika miezi ya karibuni kukubalika kwa mpango wake wa kuandaliwa Kombe la Dunia baada ya miaka miwili lakini amekumbwa na ushindani kutoka Ulaya na Amerika Kusini.

CAF pia inatarajiwa kuomba idhini rasmi ya mipango ya kuandaa Super League – wazo jingine la Infantino – ambayo itashuhudia ratiba ya kudumu ya timu 20 huku kukiwa na mabadiliko mara moja au mbili kila msimu.

"Super League ya Afrika ni mashindano mapya kwa sababu mashindano mengine hayo yote yamefunganishwa na mikataba na fedha zinazopatikana hazitoshi,” alisema Motsepe.

Mipango sawa na hiyo barani Ulaya ilishindwa vibaya sana lakini, licha ya hili, Afrika imeshinikiza kuundwa ligi hii barani humo.

Reuters