BVB mabingwa wa kombe la Ujerumani | Michezo | DW | 28.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

BVB mabingwa wa kombe la Ujerumani

Borussia Dortmund imefikisha mwisho vipigo katika fainali tatu zilizopita za kombe la DFB Pokal na kunyakua mara hii kombe  hilo kwa kuishinda Eintracht Frankfurt 2-1

Deutschland Borussia Dortmund gewinnt den DFB-Pokal (Reuters/F. Bensch )

Kocha wa Borussia Dortmund Thomas Tuchel

Bao  la  mkwaju  wa  penalti  katika  dakika  ya  67  la Pierre-Emerick Aubameyang  lilitosha kuipa ubingwa  Dortmund. Ilikuwa taji  la  kwanza  kubwa  kwa  mshambuliaji  huyo  kutoka Gabon  akiwa  na  Dortmund, lakini  inawezekana  kuwa ni  mara  ya  mwisho  kwa  mchezaji huyo  kuonekana  katika  sare  za  BVB baada  ya  kusema  ataamua  hatima  yake  baada ya  mazungumzo  na  viongozi  wa  klabu  hiyo.

Deutschland Dortmund gewinnt den DFB-Pokal (picture alliance/GES/M. Ibo Güngör)

Borussia Dortmund wakishangiria ushindi wa kombe la DFB mjini Berlin 2017

Ushindi  wake  wa  kombe  la  Ujerumani  unakamilisha  msimu  wa  mafanikio  kwake binafsi  wa  mabao  40  katika  mashindano  yote  aliyoshiriki, ikiwa  ni pamoja  na kumshinda  mshambuliaji  wa  Bayern Munich Robert Lewandowski  na  kuwa  mfungaji  bora katika  Bundesliga  akiwa  na  mabao  31.

Ushindi  huo  umekamilisha  hali  ya  mabadiliko  kwa  Dortmund  ambayo  msimu  huu ulishanza  kuonekana umeharibika  kufuatia  shambulio  la  bomu  katika  basi  la  timu  hiyo mwezi  Aprili  ambapo  mlinzi  wa  Dortmund Marc Bartra  alijeruhiwa  na  wachezaji  kupata fadhaa.

Deutschland Dortmund gewinnt den DFB-Pokal (Reuters/B. Thissen)

Aubameyang pamoja na wachezaji wa Dortmund wakishangiria ushindi wa DFB Pokal

Mapambano yaliendelea

Lakini  kocha  Thomas Tuchel  aliendelea  kuwapa  machezaji  wake  motisha  na  ari  ya kucheza  hadi  mwisho.

"Nimepwelewa, sina  nguvu  tena  sasa,"  amesema  Tuchel , ambaye  hatima  yake  katika klabu  hiyo  haifahamiki  baada  ya  mzozano  na  wakubwa  wake  katika klabu. "Ilikuwa  ni kazi  ngumu lakini  tumefanikisha."

"Baada  ya   kile  kilichotokea katika  shambulio na  kuweza  kuepuka  vikwazo  kila  mara  na kisha  kuja  hapa na  kushinda  ni  kitu  mahsusi  kabisa kwetu  sisi,"  alisema , na  kuongeza angependa  kubakia  Dortmund. "ndio , bila  shaka  ningependa  kubakia."

Deutschland Dortmund gewinnt den DFB-Pokal | Reus und Schürrle (Reuters/F. Bensch)

Marco Reus (kushoto) na Andre Shuerrle wa Dortmund wakiwa na kombe la Ujerumani DFB Pokal , 2017

Lilikuwa  ni  taji  la  kwanza  kwa  Tuchel , ambae  alijiunga  na  Borussia  Dortmund  mwaka 2015, na  kwa mshambuliaji  wa  pembeni  Marco Reus , anaonekana  kuwa  miongoni  mwa wachezaji  wenye  vipaji  vya  juu  kabisa  katika  kizazi  chake , lakini  ambaye  amepoteza fainali  nne  tangu  kuwasili  mwaka  2012  katika  kikosi  cha  BVB, ikiwa  ni  pamoja  na fainali  ya  Champions League  ya  mwaka  2013.

Ushindi  wa  Dortmund  pia  una  maana  kwamba  Freiburg , iliyoshika  nafasi  ya  7  katika msimamo  wa  ligi  ya  Ujerumani  Bundesliga , itashiriki  katika  ligi  ya  Ulaya  katika  awamu ya  mchujo.

Deutschland Dortmund gewinnt den DFB-Pokal | Marc Bartra (Reuters/F. Bensch)

Marc Bartra mlinzi wa Borussia Dortmund akishangiria pamoja na mashabiki

Mchezo ulikuwa wa vuta nikuvute

Dortmund  ilianza  kwa  nguvu  mwanzoni  mwa  mchezo  huo wakati  Dembele  alipokea pasi  kutoka  kwa  Lukasz Piszczek upande  wa  kulia na  kumpiga  chenga  mlinzi  kabla  ya kuuzungusha  mpira  huo  na  kutumbukia  wavuni  na  kuandika  bao  la  kwanza  kwa Borussia.

DFB Pokal Finale Eintracht Frankfurt Fans vor dem Spiel ( Reuters/K. Pfaffenbach)

Mashabiki wa Eintracht Frankfurt pia walishamiri katika fainali hiyo mjini Berlin

Frankfurt  ilihitaji  muda  kuweza  kurejea  katika  hali  yao  ya  kawaida  baada  ya  bao  hilo na  walifanya  hivyo  katika  fursa  yao  ya  kwanza  wakati  Rebic alipopewa  pasi  safi kutoka kwa  Mijat Gacinovic  na  kuutumbukiza  mpira  wavuni  akimwacha 

mlinda  mlango Roman Buerki  akigaaga.

Karibu  Frankfurt wapate  bao  la  pili  katika  dakika  ya  39 lakini  shuti  la  chini  la  Haris Severovic  liligonga  mlingoti  wa  goli wakati  Dortmund  walisubiri  kwa  hamu  mapumziko.

Fußball Trainer Nico Kovac Eintracht Frankfurt (Imago/Matthias Koch)

Kocha wa Frankfurt Niko Kovac

"Tulicheza  mchezo  mzuri katika  muda  wote  wa  dakika  90,"  alisema  kocha  wa  Frankfurt Niko Kovac. "Walikuwa  wazuri katika  kipindi  cha  pili. Mambo  fulani  yanaamua  fainali. Tulipiga mpira  katika  mlingoti  wa  goli, na  kisha  ikaja penalti  dhidi  yetu."

Dortmund  ilipata  mkwaju  wa  penalti  katika  dakika  ya  67 na  Aubameyang , aliukwamisha mpira  huo  wavuni  na  kuhitimisha  msimu  wenye  kumbukumbu  kadhaa .

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri:

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com