1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BVB kidedea, Bayern hoi

Sekione Kitojo
4 Februari 2019

Mabingwa  watetezi  wa  Bundesliga Bayern  Munich yateleza kwa kipigo dhidi ya Leverkusen Borussia  Dortmund yatoka  jasho mjini  Frankfurt yaambulia sare.

https://p.dw.com/p/3ChN4
Bundesliga 20. Spieltag | Eintracht Frankfurt vs. Borussia Dortmund | 1. TOR Dortmund
Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Borussia  Dortmund  ilipanua  uongozi wake  juu  ya  msimamo  wa ligi  kwa  pointi  moja  zaidi  hadi  pointi saba  sasa  baada  ya  kutoka  sare  ya  bao 1-1  na  wenyeji Eintracht  Frankfurt  mjini  Frankfurt.  BVB  huenda  imepoteza pointi mbili  muhimu mjini  Frankfurt  lakini  Marco  Reus  anaendelea kupachika  mabao , na  goli  lake  la  13  siku  ya  Jumamosi  lilikuwa na  maana  huu  ni  msimu  wake  mzuri  kabisa  baada  ya  michezo 20  ya  ligi.

Bundesliga 20. Spieltag | Eintracht Frankfurt vs. Borussia Dortmund
Marco Reus wa BVB akielekeza jambo kwa wachezaji wenzakePicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Licha  ya  kupoteza  nafasi  kadhaa  kuongeza  idadi  ya mabao  yake  katika  mchezo  huo , kama  ilivyokuwa  wiki  moja kabla  dhidi  ya  Hannover 96, Reus  yuko  njiani  kuipiku rekodi yake ya  msimu  wa  2011/12 alipofunga  mabao 18 wakati  akicheza katika  kikosi  cha  Borussia  Moenchengladbach. Mbinyo  kwa mabingwa  watetezi  Bayern  Munich unaongezeka  baada  ya kukubali kipigo  cha mabao  3-1  dhidi  ya  Bayer 04 Leverkusen siku  ya  Jumatatu  ambayo  ilishuhudia  ikiporomoka  hadi  nafasi ya  tatu  katika  Bundesliga.

Mabingwa  hao  watetezi  wanakabiliwa  na mapambano  magumu katika  wiki  hizi mbili  wakati  katikati  ya  wiki  hii  inakabiliana  na Hertha  Berlin  katika  kombe  la  Ujerumani , DFB Pokal  ikifuatiwa na  mchezo  wa  duru  ya  kwanza  ya  Champions League  duru  ya mtoano  ya  timu  16  dhidi  ya  Liverpool  ya  Uingereza  baadaye mwezi  huu.

Deutschland Leon Bailey
Leon Bailey wa Leverkusen akishangilia bao lake la kusawazisha dhidi ya Bayern MunichPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Kocha  Niko  Kovac  wa  Bayern  alikuwa  hana  jibu  dhidi  ya  kikosi cha  kocha  Peter Bosz  wa Leverkusen  licha  ya  kuanza kulifumania  lango  la  wenyeji  katika  dakika  ya  41  ya  mchezo.

Gladbach yachupa

Borussia  Moenchengladbach  ilichupa  na  kuipita  Bayern  Munich katika  msimamo  wa  ligi  na  kuchukua  nafasi  ya  pili  kwa  wingi wa  magoli, timu  zote  zikiwa  na  pointi 42  kutokana  na  michezo 20 ya  Bundesliga  hadi  sasa. Kwa  mara  ya  kwanza   katika miaka  33, Gladbach  imeweza  kushinda  michezo  mitatu  ya mwanzo  ya  mwaka .

Fußball Trainer Niko Kovac Bayern München
Kocha wa bayern Munich Niko KovacPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Pia  ni  pointi  zake  nyingi  kutia  kibindoni katika  michezo 20 tangu  msimu  wa mwaka  1969/70  na  tena msimu  wa  mwaka  1976/77 wakati  katika misimu  yote  hiyo iliweza  kumaliza  kwa  kushinda  taji  la  ubingwa  wa  Bundesliga. Kikosi  cha  kocha  Dieter Hecking  cha  Gladbach  pia  ni  timu pekee  ambayo nyavu  zake  hazijatikiswa  katika  Bundesliga  tangu kuanza  mwaka  huu  wa  2019.

Kwa upande  wa  kombe  la  Ujerumani , timu  zitawania  kuingia katika  duru  ya  robo  finali  kuanzia  kesho  ambapo  mabingwa mara  nne  Borussia  Dortmund  watakuwa  na  ndoto  ya  kupata mataji  mawili  ya  nyumbani  kama  mwaka  2012  wakati watakapoikabili  Werder Bremen  katika  mchezo  wao  wa  duru  ya timu  16  kesho  Jumanne.

Dortmund  imecheza  katika  kila  fainali tangu  mwaka  2011  wakati  RB Leipzig  ina  lenga  kuingia  katika robo  fainali  yake  ya  kwanza  wakati  watakapokumbana  na mabingwa  wa  mwaka  2015 Wolfsburg siku  ya  Jumatano.

Fußball Bundesliga Hannover 96 - RB Leipzig
Wachezaji wa kikosi cha RB LeipzigPicha: picture-alliance/dpa/S. Pförtner

Pambano  lingine  la  timu  za   ligi  daraja  la  kwanza  katika Bundesliga  ni  kati  ya  Schalke 04  dhidi  ya  Fortuna  Dusseldorf, wakati  Hamburg  SV  iliyoko  daraja  la  pili  inapambana  na Nuremberg  ya  daraja  la  kwanza, Heidenheim  ina  miadi  na  Bayer 04  Leverkusen  na  Holstein Kiel  inaikaribisha  Augsburg, bila kusahau  pambano  la  miamba  wa  daraja  la  pili  kati ya  MSV Duisburg  dhidi  ya  Paderborn.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / rtre / ape / dpae

Mhariri: Idd  Ssessanga