Bush azuru Rwanda | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bush azuru Rwanda

Amelitembelea jumba la makumbusho ya mauaji ya kimbari

default

Rais Bush alipokuwa nchini Tanzania

Rais wa Marekani Bwana George W. Bush amewasili mjini Kigali leo Jumanne akiwa na mkewe Bi Laura Bush. Rais Bush amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Kigali akiwa na ujumbe mkubwa sana akitokea Tanzania.

Kumekuwepo na maandalizi kem kem hapo kabla ya ujio wa rais Bush, ambapo kila eneo ambalo amepangiwa kupitia limepambwa kwa bendera za nchi mbili yaani ile ya Rwanda na Marekani.

Licha ya mazungumzo na rais wa Rwanda Paul Kagame, Bush anataraji pia kulizuru jengo la makumbusho ya wahanga wa mauaji ya kimbari lililopo nje kidogo ya mji wa Kigali ambako kulizikwa masalia ya miili ya watu wapatao 250.000.

Baadaye pia atafanya mazungumzo na rais katika ikulu ya mjini Kigali kisha aelekee moja kwa moja kwenye ubalozi mpya wa Marekani ambako atauzindua rasmi ubalozi huo. Jengo hilo ni la kifahari na lilianza kutumika mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu.

Rais Bush pia anatazamiwa kuizuru shule moja ya sekondari ya mjini inayojulikana kama Lycee de Kigali, kabla ya kuelekea nchini Ghana.

Waziri wa nchi wa Rwanda anayehusika na ushirikiano wa kimataifa, Bibi Rosemary Museminali, ameitaja Marekani kama mfadhili mkuu wa Rwanda hususan kwa kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa zilizoisadia Rwanda muda mfupi baada ya mauaji ya kimbari hapo mwaka 1994.

Baadhi ya misaada ya Marekani kwa Rwanda kwa mujibu wa waziri huyo ni pamoja na ule wa kupambana na ugonjwa wa ukimwi, kifua kikuu na malaria unaojulikana kama, PEPFAR, ambao unadhaminiwa na rais Bush mwenyewe.

Amesema Marekani imekuwa mstari wa mbele kusaidia katika kuboresha kilimo cha chai na kahawa nchini Rwanda kiasi kwamba hivi sasa iwe kahawa au hata chai ya Rwanda ni miongoni mwa mazao yenye viwango bora kabisa katika soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda, Dr Charles Murigande, ziara ya rais Bush inajikita katika nchi zinazoonekana kuendesha utawala bora, uwekezaji katika elimu, kuendeleza ujasiriamali, afya na kuhifadhi mazingira.

Ameyataja makampuni kama Starbacks na Gost-co ya kimarekani ambayo yananunua kahawa na chai ya Rwanda pamoja na kuwasaidia wakulima wa mazao hayo hapa nchini.

´Marekani imekuwa ikitusaidia kupata masoko huko, inaangalia ni wapi tunaweza kuwekeza katika nchi hiyo na wao kuchunguza maeneo ambayo wanaweza kuwekeza mali zao. Wote tumekuwa tukishirikiana pamoja kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mazingira mema ya kuwekeza katika nchi mbili. Tunaamini tunapofanya hivi si huko Marekani peke yake isipokuwa hata katika nchi nyingine. Hakika tunao uhusiano mzuri.´

Rais George W Bush ziara yake ya siku sita katika bara la Afrika aliianzia nchini Benin,Tanzania, kabla kuzuru Rwanda hii leo. Leo hii jioni anatazamiwa kuwasili nchini Ghana hatimaye kumalizia nchini Liberia.

 • Tarehe 19.02.2008
 • Mwandishi Christopher Karenzi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D9sw
 • Tarehe 19.02.2008
 • Mwandishi Christopher Karenzi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D9sw
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com