Bush alinganisha Iraq na Vietnam | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 22.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Bush alinganisha Iraq na Vietnam

Ni juu ya Wairaki wenyewe kumwondosha waziri mkuu Nuri al-Maliki au la – haya aliyasema rais George W. Bush wa Marekani. Wakati huo huo alimtaka al-Maliki kufanya zaidi kuleta amani kati ya pande zinazopigana. Katika hotuba nyingine atakayoitoa leo na ambayo ilichapishwa awali, rais Bush kwa mara nyingine tena ataonya kutoliondosha haraka jeshi la Marekani kutoka Iraq akiilinganisha hali hii na ile ya Vietnam.

Iraq inaendelea kukumbwa na mashambulio

Iraq inaendelea kukumbwa na mashambulio

Bush hajamuunga mkono wazi waziri mkuu wa Iraq al-Maliki lakini alikiri kuwa matatizo ya kufikia malengo ya kisiasa ni makubwa.

Baada ya mkutano wake na viongozi wa Canada na Mexiko uliofanyika mjini Montebello, Canada, Bush alizungumza mbele ya waandishi wa habari, na alisema: “Watu wa Iraq wamechukua hatua kubwa kuelekea maridhiano pale walipoikubali katiba ya kisasa kabisa katika eneo la Mashariki ya Kati. Lakini sasa ni juu ya serikali mpya kutekeleza sera zake. Nadhani, kwa kiwango fulani watu wamevunjwa moyo na uongozi kwa jumla, kutoweza kwake kufanya kazi, kwa mfano kuhusu kupitisha sheria juu ya kugawana mapato ya mafuta au kuwa na uchaguzi wa mikoa.”

Mapema Jumanne, balozi wa Marekani nchini Iraq, Ryan Crocker alisema maendeleo nchini humo ni ya kuvunja moyo kabisa. Mwenyekiti wa kamati ya bunge la Senate inayoshughulikia masuala ya jeshi, Bw. Carl Levin, ambaye amerudi kutoka Iraq hivi punde, alidai serikali ya al-Maliki iondoshwe madarakani kupitia uchaguzi kwa sababu imeshindwa kutafuta suluhisho juu ya masuala muhimu ya kisiasa.

Bush lakini alisisitiza kuwa hatua fulani zimechukuliwa na alikumbusha kuwa kubadilisha serikali ni uamuzi unaopaswa kuchukuliwa na Wairaqi na siyo na wanasiasa wa Marekani.

Leo hii rais Bush anatarajiwa kutoa hotuba mbele ya mkutano na askari wastaafu wa Marekani. Kulingana na sehemu kadhaa ya hotuba hii zilizochapishwa awali, Bush anaonya kwamba kuondoka mapemba nchini Iraq kutazusha matatizo zaidi katika wakati ambapo majeshi ya Marekani yameanza kupata mafanikio.

Katika hotuba hiyo Bush anailinganisha hali ya Iraq na ile ya Vietnam ambapo mamia ya maelfu ya watu wameuawa baada ya jeshi la Marekani kuondoka. Wengi walisema sisi kuondoka hakutakuwa na athari kwa watu wa Vietnam, hatuba hii inasema. Lakini dunia iliwahi kuona vile makadirio haya yalivyokuwa kosa kubwa.

Bush atataja pia kwamba historia ya Vietnam na kuondoka kwa Marekani nchini humo inatumiwa na magaidi wenye lengo la kuongeza chuki dhidi ya Marekani. Kwa mujibu wa hotuba yake, Bush anaongeza kusema kuwa jibu lake ni wazi: Serikali yake itaendelea kuyaunga mkono majeshi yake na makamanda wake na kuwapa kile wanachokihitaji.

Wakati huo huo, Iraq leo hii imekumbwa na mashambulio mengine mabaya. Kaskazini mwa nchi hiyo, wanajeshi 14 wa Marekani walikufa katika ajali ya helikopta. Na watu wasiopungua 20 waliuawa katika shambulio la kujitoa muhanga karibu na mji wa Baiji ambapo mshambuliaji aligongana na tangi la mafuta mbele ya kituo cha polisi.

 • Tarehe 22.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB1q
 • Tarehe 22.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB1q

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com