1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yatuma vikosi vyake mashariki mwa DRC

15 Agosti 2022

Burundi imeanza kuwatuma wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusaidia kurejesha amani katika eneo hilo linalozongwa na machafuko.

https://p.dw.com/p/4FYti
Somalia - Amison Soldaten  aus Burundi in Mogadishu
Picha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limesema hatua ya Burundi ni sehemu ya makubaliano yaliyoungwa mkono na nchi saba za kanda hiyo.

”Vikosi vya ulinzi vya Burundi vimeanza kuingia rasmi DRC leo… chini ya mpango ulioridhiwa na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC,” amesema Luteni Marc Elongo ambaye ni msemaji wa jeshi katika mkoa wa Kivu Kusini.

Kikosi hicho kinachojumuisha "idadi kubwa ya wanajeshi”, kiko chini ya kamandi ya vikosi vya Jamhuri ya Congo ambayo kwa sasa iko kwenye chuo cha mafunzo cha kijeshi kilichoko Uvira, aliliambia shirika la habari la AFP.

Wanajeshi wa Burundi pamoja na wenzao wa Jamhuri ya Congo wamepewa jukumu la kuyasaka makundi yote ya kigeni ambayo yanamiliki bunduki eneo hilo, na kurudisha utulivu mashariki mwa Congo, amesema.

Jenerali Ramazani Fundi, mkuu wa operesheni za kijeshi Kivu Kusini amehimiza umma ”kuwa na utulivu na ushirikiane na vikosi tiifu ili kuyatokomeza mashambulizi yanayofanywa na wanamgambo,” amesema Elongo.

Mnamo Juni, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walibuni kikosi cha kikanda kufanya kazi na jeshi la DRC kukabiliana na makundi yenye silaha yanayovuruga amani mashariki mwa Congo.

Makundi yenye silaha yamesheheni mashariki mwa DRC

yapo zaidi ya makundi 120 ya wanamgambo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo yamekuwa yakifanya mashambulizi dhidi ya raia.
yapo zaidi ya makundi 120 ya wanamgambo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo yamekuwa yakifanya mashambulizi dhidi ya raia.Picha: picture-alliance/dpa/AFP/E. Goujon

Takriban makundi 120 yenye silaha yamekuwa yakifanya mashambulizi katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini. Mengi ya makundi hayo yana uzoefu mkubwa wa vita vilivyoshuhudiwa katika miaka ya mwisho ya karne ya 20.

Wazo la kuanzisha kikosi cha kikanda limekosolewa ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wapinzani wa mpango huo wametaja visa vya zamani vya nchi za nje kuingilia masuala ya ndani ya Congo, badala yake wanashinikiza mageuzi na serikali kuyafadhili vyema majeshi ya Congo.

Wakosoaji hao akiwemo mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018, daktari Denis Mukwege, mtaalamu wa matibabu ya wanawake ambaye amewatibu maelfu ya wanawake ambao ni waathiriwa wa ubakaji katika eneo hilo la machafuko.

Nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

(AFPE)