1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yatangaza kutonyamaza ikishambuliwa na Rwanda

9 Desemba 2025

Waziri wa mambo ya kigeni wa Burundi amesema kamwe nchi yake haitoendelea kunyamaza ikiwa Rwanda itaendelea kushambulia ngome za vikosi vya Burundi vilivyopelekwa kusimamia amani mashariki mwa DRC.

https://p.dw.com/p/550Kf
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Wanajeshi wa Burundi wakiwa Minova
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanajeshi wa Burundi wakiwa MinovaPicha: ALEXIS HUGUET/AFP

Waziri Edourd Bizimana aliyasema hayo katika mkutano na mabalozi wa nchi za kigeni na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa nchini Burundi, na kueleza kuwa Wakongomani zaidi ya elfu 3,400 wamekimbilia Burundi katika siku mbili zilizopita.

Katika mkutano huo, Waziri Bizimana alisema licha ya Rwanda kutia saini makubaliano ya amani, inaendelea kushambulia ngome za majeshi ya Burundi mashariki mwa DRC.

Madai ya Rwanda kutumia droni na makombora maeno ya Ruvungi na Uvira

Amesema wanajeshi wa Rwanda wametumia makombora na ndege zisizokuwa na rubani katika maeneo ya Ruvungi na Uvira, na kwamba operesheni hiyo ilikusudia makubaliano ya Washington yasainiwe huku wakiwa tayari wameteka maeneo hayo. "Walitumia ndege zisizokuwa na rubani, makombora makubwa yaliwashambulia raia katika maeneo yao; wengi waliuawa na wengine kulazimika kukimbia. Hivi tumekwisha kupokea watu zaidi ya elfu 3,400 raia wa DRC waliokuja Burundi kuanzia tarehe 06 hadi 07 mwezi huu wa Desemba.”

Picha ya mchanganyiko | Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye – Rais wa Rwanda Paul Kagame.
Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye na Rais wa Rwanda Paul Kagame.Picha: Rafiq Maqbool/Alberto Pezzali/AP/picture alliance

Miongoni mwa waliotoroka mashambulizi ni pia raia wa Burundi. Waziri Bizimana amesema familia zaidi ya 1,300 za Warundi waliokuwa wakiishi mashariki mwa DRC wamekimbilia Burundi.

Mashambulizi yaelezwa kufanyika katika ardhi ya Burundi

Aidha, amesema makombora mawili yaliangukia upande wa Burundi katika tarafa ya Cibitoke, eneo linalopakana na Congo, na kuwajeruhi watu wawili: mtoto wa miaka 12 na mwanamke.

Licha ya mapigano kuendelea, Waziri Bizimana amesema mipaka ya Burundi inaendelea kulindwa. "Wanajeshi wetu wamesimama vizuri na wamekuwa wakiwarudisha nyuma wanaoshambulia. Sisi tunafuatilia kwa karibu hali ya mambo; hatutaki vita, tunapendelea kuishi vizuri na majirani zetu, lakini atakayevuruga usalama wa raia wa Burundi au kushambulia majeshi yetu tuliyoyapeleka hatuwezi kuvumilia. Tutajihami bila kusita.”

Uhusiano kati ya Burundi na Rwanda umedorora tangu 2015, na kusababisha mipaka ya nchi hizo mbili kufungwa. Wiki iliyopita, Rais Évariste Ndayishimiye alisema mpaka wa Burundi utafunguliwa pale Rwanda itakapowarejesha wakimbizi wanaohusishwa na jaribio la mapinduzi la Mei 2015 nchini Burundi.

DW – Bujumbura