Burundi yapuuza nguzo muhimu ya amani | Matukio ya Afrika | DW | 12.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Burundi yapuuza nguzo muhimu ya amani

Wanadiplomasia wa juu wameonya kuwa serikali ya Burundi imeonyesha nia ya kuondoa viwango vya uwakilishi wa makabila katika nafasi za uongozi, ambao ni nguzo muhimu ya makubaliano ya amani yaliokomesha vita vya miaka 13

Wanadiplomasia hao kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Ubelgji na Marekani, wamezitolea mwito pande zote kushiriki mjadala wa wazi, mpana na shirikishi wa kisiasa.

Katika taarifa yao ya pamoja, wanadiplomasia hao wamesema kufuatia miezi kadhaa ya machafuko na mchakato wa uchaguzi uliogubikwa na utata, serikali ya Burundi inaweza tu kuanza kurejesha imani kupitia mjadala wa kisiasa unaovishirikisha vyama vyote vya kisiasa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa serikali ya Burundi haiwezi kumudu kuendelea na njia inayoelekea zaidi kwenye ukosefu wa utulivu, migawanyiko na kuporomoka kwa uchumi wa nchi na migogoro ya kibninaadamu.

Hofu imetanda juu ya kuripuka upya kwa vita nchini Burundi.

Hofu imetanda juu ya kuripuka upya kwa vita nchini Burundi.

Hofu ya kurejea vitani

Kuna hofu kubwa ndani na nje ya Burundi, kwamba taifa hilo dogo lililoko katikati mwa kanda ya maziwa makuu, huenda likatumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Vita vya mwisho nchini Burundi, ambavyo vilimalizika mwaka 2006 viliuwa watu wasiopungua 300,000.

Lakini wanadiplomasia hao wameonya kwamba serikali ilikuwa inapuuza nguzo muhimu ya makubaliano ya mwaka 2000 yaliyosafisha njia ya kumalizika kwa vita, kwa kuondoa viwango vya uwakilishi katika nafasi muhimu za serikali, kati ya Wahutu walio wengi, na Watusti walio wachache.

Wanadiplomasia hao wamesema kukomeshwa wiki iliyopita, kwa urari wa kijinsia katika kamati ya uongozi wa bunge, kunaonyesha nia inayotatiza ya chama tawala kufuta moja ya kanuni muhimu za amani na utulivu, zilizoiwezesha Burundi kutoka kwenye vita vya muda mrefu.

Taarifa hiyo ya pamoja imetolewa nchini Kenya na mjumbe wa Umoja wa Mataifa Said Djinit, mjumbe wa Umoja wa Afrika Ibrahim Fall, mjumbe wa Marekani Thomas Perriello, Koen Vervaeke kutoka Umoja wa Ulaya na Frank De Conick kutoka mkoloni wa zamani wa Burundi, Ublegji.

Wakimbizi wa Burundi wlioko nchini Tanzania.

Wakimbizi wa Burundi wlioko nchini Tanzania.

Maelfu wameikimbia nchi

Uchumi wa Burundi, ambao ni moja ya chumi dhaifu zaidi duniani, umeshuka zaidi katika miezi ya karibuni, na unaonyesha dalili ndogo sana za kufufuka wakati kukiwa hakuna suluhisho la mgogoro unaoendelea kuikabili, wamesema wanadiplomasia hao. Tayari maelfu wamekimbilia katika nchi jirani za Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Wameongeza kuwa mjadala utakaopeleea kuwepo na suluhu ya muafaka kwa machafuko nchini Burundi ndiyo njia bora ya kuwahamasisha wakimbizi kurejea nyumbani na kuepusha kuivuruga kanda nzima.

Umoja wa Mataifa ulisema siku ya Jumanne kuwa umesha sajili zaidi ya wakimbizi 181,000 wa Burundi katika mataifa jirani, lakini idadi ya waliokimbia inaonekana kuwa kubwa zaidi.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya kibinaadamu OCHA, ilisema wafanyakazi wa misaada tayari wameanza kuweka akiba ya chakula na mahitaji mengine, katika kujiandaa na kuporomoka zaidi kwa hali ya kibinaadamu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Josephat Nyiro Charo