Burundi imesimama njia panda | Matukio ya Afrika | DW | 10.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Burundi imesimama njia panda

Serikali ya Burundi imewaamuru watu waache kuandamana dhidi ya uamuzi wa Rais Nkurunziza wa kuwania muhula wa tatu wa Urais. Serikali hiyo imewataka waandamanaji na viongozi wao waache harakati zao mara moja .

Waandamana kumpinga Nkurunziza nchini Burundi

Waandamana kumpinga Nkurunziza nchini Burundi

Baraza la usalama la kitaifa nchini Burundi limesema watu hao waache uasi wao unaoyatatiza maisha ya watu wa Burundi. Waandamanaji wamepewa muda wa saa 48 kiviondoa vizuizi vyote walivyoviweka barabarani.

Baraza hilo la usalama linaloongozwa na Rais Nkurunziza limetaka njia zote zilizowekewa vizuizi na wapinzani hapo awali zifunguliwe na majeshi ya usalama, katika muda wa saa 48.

Lakini kiongozi wa upinzani Pacifique Nininahazwe ameishutumu amri hiyo iliyotolewa na serikali na ameiita kuwa ni tangazo la vita. Bwana Nininahazwe amesema maandamano yataendelea hadi hapo Rais Nkurunziza atakapouacha mpango wake wa kuwania muhula wa tatu wa urais unaoenda kinyume na katiba ya nchi.

Waandamanaji wasimamisha harakati kwa muda baada ya watu 18 kufa

Hata hivyo wanaandamanaji hapo jana walisimamisha harakati zao kwa siku nzima na kuwezesha utulivu kurejea katika mji mkuu wa Burundi,Bujumbura. Waandamanaji wamezisimamisha harakati zao kwa mara ya kwanza baada ya wiki kadhaa.

Mpaka sasa watu zaidi 18 wameshakufa, miongoni mwao polisi na waandamanaji, tangu tarehe 26 ,siku ambapo Rais Nkurunziza alitangaza dhamira ya kuwania kipindi cha tatu cha urais. Rais Nkurunziza ameshutumiwa kwa uamuzi wake na nchi kadhaa ikiwa pamoja na Marekani.Umoja wa nchi za Afrika pia haujaridhika na uamuzi wa Rais huyo. Uchaguzi wa rais nchini Burundi unatarajiwa kufanyika mwezi ujao. Wapinzani wanasema uamuzi wa Nkurunziza unakiuka katiba na pia mkataba wa amani uliovimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.

Rais Nkurunziza asonga mbele na uamuzi wake

Burundi Präsident Pierre Nkurunziza

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza

Ijumaa iliyopita Rais Nkurunziza aliwasilisha rasmi hati za kumwezesha kusimama katika uchaguzi. Nkurunziza alienda mwenyewe kujiandikisha kwenye tume ya uchaguzi.

Lakini hatua yake ilifuatiwa na ile ya kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa.Viongozi wengine wa upinzani pia walijiandikisha.

Bwana Rwasa amesema kujiandikisha kwake hakuna maana ya kuukabali mchakato wa uchaguzi na wala hakuna maana ya kumkubali Nkurunziza kusimama katika kinyang'anyiro cha uchaguzi. Rwasa amesema hali ya usalama ni mbaya na amedai kwamba tawi la vijana katika chama kinachotawala ,CNDD-FDD wanaojulikana kama Imbonerakure wana silaha na wanavaa sare za polisi.

Amesema vijana hao hapo awali pia walitumiwa kuwatisha watu. Kiongozi huyo wa upinzani ameuliza vipi itawezekana kufanya kampeni katika mazingira kama hayo?

Shule zote kufunguliwa jumatatu

Wakati huo huo Baraza la Usalama la kitaifa nchini Burundi limeahidi kwamba shule zote, vyuo vikuu na ofisi za serikali zitaanza kurejea katika shughuli za kawaida hapo Jumatatu. Rais Pierre Nkurunziza pia ameahidi kwamba uchaguzi wa mwezi ujao utafanyika vizuri licha ya upinzani dhidi ya uamuzi wake wa kuwania muhula wa tatu.

Na habari zaidi zinasema,kutokana na wasi wasi, viongozi wa nchi za Afrika Mashariki watakutana nchini Tanzania Jumatano ijayo ili kuujadili mgogoro wa nchini Burundi.

Mwandishi:Mtullya Abdu.afp/rtre,

Mhariri: Sudi Mnette