1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni baada ya onyo la Ufaransa na Marekani kuhusu ugaidi

9 Julai 2010
https://p.dw.com/p/OFPZ
Jangwa la Sahara ambako vitendo vya utekaji nyara wageni na kudai fidia ya fedha vimeshamiri.Picha: picture-alliance/ dpa

Burkina faso imewahakikishia wageni wanaoizuru nchi hiyo ya Afrika Magharibi juu ya usalama wao, baada ya Ufaransa kutoa onyo kuwa raia wake wanaokwenda Afrika kaskazini, huku Marekani ikiwahamisha raia wake kutoka eneo hilo kutokana na hofu ya mashambulio ya wanaharakati wa kiislamu.

Burkina faso ni nchi ya karibuni katika eneo la Afrika magharibi kukabiliwa na kitisho cha tawi la kundi la kigaidi la Al Qaeda katika Afrika Kaskazini, ambalo limelitumia eneo kubwa la jangwa katika ukanda huo kuimarisha vitendo vya utekaji nyara wageni na mashambulio dhidi ya wanajeshi .

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Burkina faso, Alain Yoda,amesema hadi sasa hatua za usalama za nchi yake zimeonyesha zinafanya kazi barabara, akisema hakuna tatizo lolote, ingawa kila mtu anapaswa kuchukua hatua za tahadhari zinazohitajika kwa usalama .

Mapema mwezi huu, ubalozi wa Marekani ulionya kwamba Waislamu wa itikadi kali walikuwa wakipanga kuwateka nyara wageni, na wiki iliopita ubalozi wa Marekani mjini Ouagadougou ukawahamisha raia wake kutoka kaskazini mwa mji mkuu huo , wengi wakiwa ni watumishi wa kujitolea wa shirika la Peace Corp.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa nayo ikitoa mfano wa vitisho vya kigaidi nchini Mali na Niger, pia imewaonya raia wake kutosafiri katika maeneo ya kaskazini mwa Burkina faso.

Wakati Burkina faso haikukanusha ripoti zilizosababisha Marekani kuchukua hatua za usalama, Waziri wa nje wa Burkina faso alisema pamoja na hayo hazikutokana na idara ya usalama ya Burkina faso, hivyo hangewashauri wageni wasisafiri katika sehemu za kaskazini mwa nchi hiyo. Alisema hakuna hata kitendo kimoja cha utekaji nyara kilichofanywa ndani ya ardhi ya Burkina faso.

Hata hivyo, onyo lililotolewa kwa raia hao wa kigeni linatokana na hali ya kwamba mikoa ya kaskazini mwa Burkina faso iko karibu na Mali na Niger, waliko wanaharakati hao wa Kiislamu .Kutokana na kitisho hicho, mataifa hayo yameathirika kwa upande wa utalii.

Mwezi Mei mwaka huu, Burkina faso ilikuwa mwenyeji wa mazoezi ya kijeshi yalioongozwa na Marekani juu ya kupambana na ugaidi, ambayo lengo lake ni kuimarisha ushirikiano dhaifu wa kimkoa kuhusiana na suala hilo na kuzuwia makundi hayo kuligeuza eneo la jangwa la Sahara kuwa mahala pao pa hifadhi sawa na inavyotokaea Yemen au Somalia.

Lakini wachambuzi wanasema suala kuu ni kwamba uhalifu unaofanywa wa utekaji nyara hufungamanishwa na mapato ya fedha nyingi zinazopatikana, pamoja na uvushaji bidhaa, kinyume cha sheria-kuanzia sigara hadi madawa ya kulevya. Ingawa haikuthibitishwa rasmi, duru za usalama zinasema utekaji nyara mara nyingi humalizikia kwa wahalifu kulipwa fidia ya mamilioni ya dola kuwaachia mateka wao.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman /Reuters

Mhariri: Miraji Othman