Burhan awaondoa mabalozi 6 kwa kukosoa mapinduzi Sudan | Matukio ya Afrika | DW | 28.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Burhan awaondoa mabalozi 6 kwa kukosoa mapinduzi Sudan

Kiongozi wa jeshi nchini Sudan amewasimamisha kazi mabalozi sita wakiwemo mabalozi wa Marekani, Umoja wa Ulaya na Ufaransa baada ya mabalozi hayo kulaani hatua ya jeshi kuidhibiti nchi.

Wanadiplomasia hao wameapa kuiunga mkono serikali iliyopinduliwa madarakani ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok. Wengine waliofutwa kazi na kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah Burhan hapo jana jioni ni mabalozi wa Qatar, China na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva, hii ikiwa ni kulingana na afisa ambaye hakutaka kujulikana.

Mabalozi hao walifutwa kazi siku mbili baada ya Jenerali Burhan kuivunja serikali ya mpito na kumzuwiya Waziri Mkuu, maafisa wengi wa serikali na viongozi wa kisiasa katika mapinduzi yaliokosolewa na Jumuiya ya Kimataifa. Hata hivyo Jeshi liliridhia Hamdok kurejea nyumbani hapo jana baada ya shinikizo za kimataifa kutaka Waziri Mkuu huyo aachiliwe huru.

Jenerali Abdel Fattah Burhan amesema jeshi liliamua kuchukua madaraka kwasababu ya migongano iliyokuwepo kati ya vyama vya kisiasa anayodai ingeliweza kuitumbukiza nchi katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Mapinduzi yaliyofanyika siku nne zilizopita yametokea wiki kadhaa kabla Burhan kukabidhi madaraka ya Baraza la uongozi kwa uongozi wa kiraia. Baraza hilo ndilo linalotoa uamuzi muhimu wa kuiongoza nchi na hatua ya kukabidhi madaraka ingelipunguza nguvu ya jeshi nchini humo. Baraza hilo lilikuwa na maafisa wa kijeshi pamoja na kiraia na serikali ya Hamdok ndio iliyokuwa ikiendesha shughuli za kiserikali.

Mapinduzi yatishia demokrasia ya Sudan

BDTD Putsch im Sudan

Baadhi ya waandamanaji Sudan

Mapinduzi haya ya kijeshi yanatishia kusitisha mchakato wa kipindi cha mpito cha Sudan kuelekea demokrasia kilichoanza baada ya kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashiri kuondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi pia baada ya maandamano makubwa dhidi yake mwaka 2019.

Kwengineko Ujumbe wa Umoja wa Ulaya ulioko Sudan umethibitisha kuwa wanadiplomasia wa kigeni wamekutana na Waziri Mkuu aliyepinduliwa Abdalla Hamdok mjini Kahartoum.

soma zaidi:Kamata kamata yaendelea Sudan baada ya mapinduzi

Katika taarifa ya pamoja na wanapiplomasia hao wakiwemo mabalozi wa Ujerumani Ufaransa Uingereza, Marekani na mataifa mengine wamesema  wamefurahi kumkuta katika hali nzuri na bado wanaendelea kutoa wito wa uhuru wake kamili.

Huku hayo yakiarifiwa  Maafisa wa afya wameripoti mauaji ya waandamanaji saba tangu jeshi lilipoipindua serikali siku ya Jumatatu. Hisham Fagiri, afisa katika wizara ya afya amesema miili mingine imewasili katika vyumba vya kuhifadhia maiti bila ya kutoa idadi kamili. Waandamanaji wanne waliripotiwa kuuwawa siku ya Jumatatu saa kadhaa baada ya mapinduzi ya kijeshi kutangazwa.

Chanzo: afp,ap, reuters