Bunge Uingereza laidhinisha Brexit | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bunge Uingereza laidhinisha Brexit

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amepata idhini ya bunge kuanzisha mchakato wa kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya (EU), na kuzima juhudi za kukwamisha mpango wake wa kuanzisha mazungumzo ya kutengana kufikia Machi 31.

Wabunge waliidhinisha mpango wa waziri mkuu May kwa kura 494 dhidi ya 122, na hivyo kumpa mamlaka ya kuanzisha mchakato wa Brexit, na kuhitimisha siku kadhaa za mjadala mkali.

Muswada huo sasa unahitaji kuidhinishwa na baraza la mamwinyi la bunge la Uingereza (House of Lords) kabla ya kuwa sheria, ambako theluthi mbili ya wabunge walipiga kampeni dhidi ya Brexit, na ambako waziri mkuu hana wingi wa wabunge.

Ushindi huo unaashiria hatua muhimu kuelekea kuanza kwa kile kinachotarajiwa kuwa majadiliano magumu na marefu na Umoja wa Ulaya kuhusu masuala kama vile biashara, uhamiaji na usalama ambavyo vitabadili jukumu la Uingereza duniani.

Baada ya kunusurika uasi mdogo ndani ya chama chake cha kihafidhina uliokuwa umetishia kudhoofisha mamlaka yake na mkakati wa majadiliano, sheria hiyo ilipita bila marekebisho yoyote na kwa wakati.

Britisches Unterhaus tagt über Brexit-Gesetz, Totale (picture-alliance/PA Wire)

Bunge la wawakilishi likijadili muswada wa sheria ya Brexit 08.02.2017

Hilo limeongeza matumaini kwamba muswada huo utapita pia kwa urahisi katika baraza kuu la bunge la Uingereza lisilo la kuchaguliwa, wakati safari yake itakapoanza huko Februari 20. Serikali inataka kukamilisha mchakato wa kisheria kufikia Machi 7.

Ushirika wa kimkakati

Waziri mkuu aliliambia bunge siku ya Jumatano kwamba wanaamini inawezakana ndani ya kipindi cha miaka miwili kufikia makubaliano siyo tu kwa ajili ya kujiondoa kwao, lakini pia ya kibiashara kuhakikisha wanaye ushirika imara wa kimkakati huko mbeleni.

Duru zilizo karibu na majadiliano katika baraza la juu la bunge zilisema wanatarajiwa kuendelea kuishinikiza serikali kulihusisha zaidi bunge wakati wa mchakato wote wa majadiliano.

Chama cha upinzani cha Labour na chama kidogo cha Scottish National Party viliwasilisha marekebisho vikitaka uthibitisho kuhusu ushiriki katika soko la pamoja, haki za wafanyakazi na za raia wa Ulaya walioko Uingereza, lakini miswada hii yote ilishindwa.

Chama cha Labour kiliwashurutisha wabunge wake kutopinga sheria hiyo, lakini 52 kati ya wabunge wake 229 walikataa kuunga mkono muswada huo, akiwemo Clive Lewis, msemaji wa kamati ya biashara ya chama hicho aliejiuzulu papo kwa hapo.

Scotland huru haiwezi kuwa ndani ya EU

Wabunge wa SNP walielezea kuvunjwa kwao moyo wakati wa kura hiyo ya Jumatano, kwa kuimba wimbo wa Umoja wa Ulaya wa "Ode to Joy" uliotungwa na Mjerumani Beethoven, kabla ya kunyamazishwa na naibu spika Lindsay Hoyle.

Mbunge wa SNP Angus Robertson alimtuhumu May kwa kushindwa kutumiza ahadi yake ya kuzihusisha Scotland, Wales na Iraland ya Kaskazini katika mchakato huo. May aliahidi kufanya kazi kwa karibu na mabunge yaliogatuliwa lakini alisema mahakama ya juu ya Uingereza iliamua kuwa mabunge hayo hayana turufu juu ya makubaliano ya Brexit.

Britisches Unterhaus tagt über Brexit-Gesetz, May (picture-alliance/PA Wire)

Waziri mkuu Theresa May akijibu maswali ya wabunge wakati mjadala kuhusu sheria ya Brexit.

"Muswada unaopitia bungeni unaipa serikali mamlaka ya kuanzisha kipengele cha 50. Na pia ningependa kumkumbusha bwana Robertson juu ya nukta hii, kwa sababu kila mara anazungumzia maslahi ya Scotland ndani ya Umoja wa Ulaya. Scotland ilio huru haitakuwa ndani ya Umoja wa Ulaya," alisema May.

UKIP washangilia

Lakini matokeo ya kura hiyo yalishangiliwa na wapiganiaji wa Brexit kama vile Nigel Farage, kiongozi wa zamani wa chama cha UK - Independence UKIP, alieandika kwenye ukurasa wake wa twitter akisema. Sikuwahi kufikiria nitaiona siku ambapo bunge la wawakilishi linapiga kura kwa wingi mkubwa kuunga mkono Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

May ameahidi kutoa kipaumbele kwa uhamiaji katika majadiliano ya Brexit, hata kama hilo linakuja kwa gharama ya kuachia uanachama wa soko la pamoja la Umoja wa Ulaya na wateja wake milioni 500.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae,rtrtv

Mhariri: Caro Robi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com