Bunge Marekani lashinikizwa kudhibiti umiliki wa bunduki | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bunge Marekani lashinikizwa kudhibiti umiliki wa bunduki

Mapendekezo mengi yamewasilishwa kupambana na udhibiti wa umiliki wa bunduki kufuatia shambulio la shule ya Florida. Marufuku ya uuzaji wa sialaha imekataliwa. Je, baraza la Congress la Marekani linaweza kuchukua hatua.

Wajumbe wa baraza la Congress la Marekani wanarejea mjini Washington Jumatatu baada ya mapumziko ya siku 10, wakiwa chini ya shinikizo la kuchukua hatua juu ya suala la vurugu zinazotokana na matumizi ya bunduki.

Mapendekezo kadhaa yaliwasilishwa kuimarisha sheria za kumiliki bunduki kufuatia shambulio la risasi la Februari 14 la shule ya sekondari ya Florida, lilosababisha vifo vya watu 17, wengi wao wanafunzi.

Rais wa Marekani Donald Trump amependekeza kuimarisha uchunguzi wa historia ya mnunuaji bunduki, kuongeza umri hadi miaka 21 wa kuweza kununua baadhi ya silaha. Lakini Trump amesema mapendekezo yote hayo yataidhinishwa na majimbo ya Marekani.

"Nimezungumza na maseneta na wabunge wa congress leo, jana, na juzi, na nadhani tutawasilisha mswada mkubwa utakaohusiana na suala la kufuatilia historia ya mnunuaji, kuondoa vitu fulani na kuweka vitu vingine, na labda tutashughulikia suala la umri, kwa sababu halionekani kuwa ni jambo la busara kwamba unapaswa kusubiri hadi miaka 21 kumiliki bastola, lakini kupata bunduki kama iliyotumiwa katika shambulizi la shule unaipata ukiwa na miaka 18," amesema Donald Trump.

USA Präsident Donald Trump in Washington (picture-alliance/AP Photo/E. Vucci)

Rais wa Marekani Donald Trump akiwa Washington

Warepublican waogopa kuwakasirisha wahafidhina wanaotetea uhuru wa kumiliki silaha

Wakiwa wanakabiliwa na uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba, wabunge wa Congress wamegawika juu ya suala hilo la udhibiti wa umiliki wa bunduki. Warepublican wanaogopa kuwashambulia wafuasi wao wa kihafidhina na watetezi wa haki za kumiliki bunduki ikiwa ni pamoja na chama chenye nguvu kinachotetea umiliki wa bunduki nchini Marekani NRA. Trump aliidhinishwa na NRA katika kampeni zake za uchaguzi wa rais wa mwaka 2016.

Chama cha NRA kimesema hakiungi mkono mapendekezo yoyote yaliotolewa na Trump na baadhi ya Warepublican wengine, huku msemaji mkuu wa chama hicho Dana Loesch akisema Jumapili kwamba chama cha NRA hakiungi mkono suala la kupiga marufuku, lakini kitaunga mkono pendekezo lenye utata la kuwapa walimu silaha.

Mswada mmoja ambao una uwezekano wa kusonga mbele ni ule unaoungwa mkono na vyama vyote viwili vya Repulican na Democratic wa kuhakikisha mashirika ya serikali ya shirikisho na majimbo yanazingatia sheria zilizopo na kuripoti taarifa za uhalifu kwa usahihi kupitia mfumo wa kitaifa wa kufuatilia historia za watu unaoendeshwa na Shirika la Kijasusi la Marekani FBI.

Mswada mwingine ambao unaweza kupata uungwaji mkono ni ule uliopendekezwa na Seneta Pat Toomey, wa Jamhuri ya Pennsylvania, na Seneta Joe Manchin, wa chama cha Democratic kutoka West Virginia, wa kupanua uchunguzi juu ya mnunuaji kabla ya ununuzi wa silaha za mtandaoni na katika maonyesho ya bunduki.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/DW http://bit.ly/2EVdkTu
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com