1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Urusi huenda likauidhinisha mkataba wa START

Kabogo, Grace Patricia23 Desemba 2010

Mkataba huo ni kwa ajili ya kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia kati ya Marekani na Urusi.

https://p.dw.com/p/zotO
Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev.Picha: AP

Bunge la Urusi limesema kuwa huenda likauidhinisha mkataba muhimu wa kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia kati ya nchi hiyo na Marekani unaojulikana kama START, mapema kesho, iwapo mkataba huo ulioidhinishwa na Baraza la Seneti la Marekani litayaacha masharti ya mkataba huo kama yalivyo.

Iwapo Urusi itauridhia mkataba huo mpya wa kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia unaojulikana kama START, kutaongeza juhudi za kuyaweka mahali pazuri mahusiano kati ya Marekani na Urusi ambayo yamekuwa siyo ya kuridhisha kwa muda mrefu. Hatua hiyo ya Urusi itakuwa ni ushindi kwa Rais Barack Obama wa Marekani na Dmitry Medvedev wa Urusi, ambao walitia saini makubaliano ya mkataba huo mwezi Aprili mwaka huu ambao umeimarisha mahusiano kati ya Marekani na Urusi.

Spika wa Bunge la Urusi, Boris Gryzlov, amesema kuwa mkataba huo lazima pia uidhinishwe na bunge la Urusi ili uweze kuanza kutumika. Bwana Gryzlov amesema kwamba huenda mkataba huo ukaridhiwa kesho Ijumaa kama Urusi itaridhika kuwa azimio la Baraza la Senete la Marekani kuuridhia hautaubadilisha mkataba huo. Spika huyo wa bunge la Urusi amesema kuna taarifa kwamba azimio hilo lina mfululizo wa masharti ambayo yameambatanishwa.

Hata hivyo, wachambuzi na wataalamu wa masuala ya udhibiti wa silaha wamesema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa mkataba huo wa START kuridhiwa na bunge la Urusi.

Baraza la Senate jana liliuidhinisha mkataba huo kwa kura 71, huku maseneta 26 wakipiga kura ya kuukataa mkataba huo ambao marais wote wawili wameiita hatua hiyo kuwa msingi mzuri katika kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia duniani kote, lengo likiwa ni kuhakikisha uwepo wa dunia isiyo na silaha za nyuklia. Aidha, mkataba huo wa START utapunguza silaha za nyuklia na kufikia 1,550 katika muda wa miaka 7.

Wakati huo huo, viongozi kadhaa duniani wameendelea kupongeza hatua hiyo ya Marekani akiwemo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague. Kwa upande mwingine, Ufaransa ambayo ina silaha za nyuklia nayo leo imeipongeza hatua hiyo ya Marekani. Ufaransa pia imetaka kuidhinishwa kwa Mkataba wa kupiga marufuku mashambulio ya mabomu ya nyuklia kwa makusudio ya kijeshi ama kiraia-CTBT, ili uweze kuanza kufanya kazi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,AFPE)

Mhariri:Josephat Charo