1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ulaya lamtambua Guaido kuwa kaimu rais Venezuela

Bruce Amani
31 Januari 2019

Bunge la Ulaya limepiga kura ya kumtambua Juan Guaido aliyejitangaza kuwa rais wa mpito nchini Venezuela na kumuongezea mbinyo Rais Msoshalisti Nicolas Maduro

https://p.dw.com/p/3CW7C
Venezuela, Caracas: Juan Guaido hält eine Rede
Picha: picture-alliance/AP/R. Abd

Wabunge wa Umoja wa Ulaya walipiga kura 429 kumuunga mkono Guaido dhidi ya 104 waliopinga, huku 88 wakijizuia kupiga katika kikao maalum mjini Brussels. Kura hiyo ni ya kiishara tu, kwa sababu bunge hilo halina usemi katika sera ya kigeni ya Umoja wa Ulaya. Bunge hilo limetoa wito kwa mataifa 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya kumtambua Guaido kuwa kaimu rais halali wa Venezuela hadi pale uchaguzi mpya wa rais ulio huru, uwazi na wa kuaminika utakapoandaliwa

Katika mahojiano yaliyochapishwa leo na gazeti la Uhispania la El Pais, Guaido amefutilia mbali uwezekano wa kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwake, akisema kuwa wananchi wengi wanamtaka Maduro ajiuzulu. Kiongozi huyo wa bunge la Venezuela ameurudia wito wake kwa jeshi la nchi hiyo kumuunga mkono.

Alijiapisha Januari 23, akisema katiba inamruhusu kuhudumu kama kiongozi wa taifa kwa sababu uchaguzi wa Maduro mwezi Mei mwaka jana haikuwa halali kwa vile wapinzani wake wakuu walizuiwa kugombea.

Venezuela Caracas Nicolas Maduro
Maduro anatafuta uungwaji mkono wa jeshi la nchiPicha: Reuters/Miraflores Palace

Wakati huo huo, Chama cha Kimataifa cha Wanahabari chenye makao yake mjini Brussels kimesema wanahabari saba wa kigeni wanazuiliwa nchini Venezuela, wakiwemo maripota wa Ufaransa na Uhispania. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametaka waachiliwe huru maramoja. Mawaziri wa Mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuujadili mgogoro wa Venezuela katika mkutano wao wa siku mbili mjini Bucharest kuanzia leo.

Nayo Urusi, ambayo inamuunga mkono Maduro, imesema leo kuwa iko tayari kusaidia kusimamia mazungumzo ya upatanishi kati ya Maduro na upinzani nchini Venezuela.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Urusi Maria Zakharova amevitaja vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela kuwa "kitendo halisi cha hujuma”

Ni Marekani tu na nchi kadhaa za Amerika Kusini zilizomtambua Guaido kuwa rais wa Venezuela. Mataifa sita ya Umoja wa Ulaya – Uhispania, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Uholanzi na Ureno – zimesema zitamtambua Guaido kuwa rais kama Maduro hatoitisha uchaguzi mpya ifikapo Jumapili wiki hii.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga