1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Marekani laidhinisha Ukraine kupewa silaha nzito

Admin.WagnerD24 Machi 2015

Wabunge wa Marekani wamepiga kura kwa wingi kumtaka Rais Barack Obama kuipa Ukraine silaha nzito ili kulinda mamlaka ya mipaka yake, dhidi ya waasi wanaopigania kujitenga , wakiungwa mkono na Urusi

https://p.dw.com/p/1Ew0K
Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Wabunge 348 dhidi ya 48 wa Marekani kutoka vyama vyote viwili vya kisiasa Democrats na Republican wameidhinisha mswada unaomshinikiza Rais Obama kuharakisha kulipa jeshi la Ukraine silaha nzito ili kuweza kupambana vilivyo na waasi wanaoungwa mkono na Urusi mashariki mwa Ukraine.

Kufuatia kukiukwa mara kadhaa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano Mashariki mwa Ukraine, kati ya jeshi la Ukraine na waasi hao wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa Ukraine, Ikulu ya Rais wa marekani mwezi huu ilitangaza itatoa msaada wa vifaa vya kijeshi visivyo vya maangamizi vya thamani ya dola milioni 75 kwa Ukraine.

Hata hivyo mnadhimu mkuu wa jeshi la Marekani Jenerali Martin Dempsey ameiambia kamati ya bunge kuhusu masuala ya ulinzi kuwa angekuwa katika nafasi ya kufanya maamuzi ya mwisho, angeipa Ukraine msaada wa silaha za maangamizi, mtazamo ambao unaungwa mkono na waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter.

Wengi waunga mkono Ukraine ipewe silaha

Spika wa bunge la Marekani John Boehner ameitaja kura hiyo kama wito wa kutaka sasa pachukuliwe hatua kwani bunge linaunga mkono pakubwa haja ya Ukraine kupewa msaada wa kijeshi.

Spika wa bunge la Marekani John Boehner
Spika wa bunge la Marekani John BoehnerPicha: picture-alliance/dpa

Mbunge wa chama cha Democrats Eliot Engel aliyeuwasilisha mswada huo bungeni amesema ni muda sasa kukoma kuuchukulia mzozo wa Ukraine kama mgogoro mwingine ulio mbali na Marekani.

Putin amekanusha kuwapa silaha waasi wa mashariki mwa Ukraine ambao walianzisha mapambano dhidi ya wanajeshi wa serikali mwaka jana wakati ambapo Urusi kulitwaa kwa nguvu eneo la Crimea kutoka kwa Ukraine.

Utawala wa Obama unatafakari hatua zaidi

Maafisa wa mambo ya nje wa Marekani wamesema utawala wa Rais Obama unajadili suala hilo la iwapo itaipa Ukraine silaha nzito za maangamizi lakini kwa hivi sasa inasubiri kuona kama makubaliano ya kusitisha mapigano na kutafuta amani yaliyofikiwa mwezi Februari katika mji mkuu wa Belarus-Minsk, yatatekelezwa kabla ya kuzingatia kuchukua hatua zaidi.

Mwanajeshi wa Ukraine katika eneo la Debaltseve
Mwanajeshi wa Ukraine katika eneo la DebaltsevePicha: Reuters/G. Garanich

Wakati huo huo, kamati ya ulinzi ya bunge la Uingereza imesema nchi hiyo inapaswa kujenga upya kwa dharura uwezo wake wa kijeshi uliopuuzwa tangu kukamilika kwa vita baridi ili kujitayarisha kukabiliana na vitisho vya kijeshi vikiwemo vile vya kutoka Urusi.

Kamati hiyo imesema Uingereza inapaswa iimarishe uwezo wake wa kinyuklia, kuziweka tayari ndege, meli za kivita pamoja na vifaru ili kumzuia Putin kuendeleza ubabe kama unaoshuhudiwa Ukraine na kuongeza ni wazi kwamba Urusi ina nguvu za kijeshi kwani ina uwezo wa kutuma wanajeshi 150,000 vitani katika kipindi cha saa 72 huku jumuiya ya kujihami ya NATO itachukua miezi sita kuweza kufanya hivyo.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman