1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Libya lateua jina la Waziri Mkuu mpya

Amina Mjahid
10 Februari 2022

Bunge la Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi, limemteua Fathi Bashagha waziri wa zamani wa mambo ya ndani kuwania nafasi ya waziri mkuu, na kuibua changamoto kwa waziri mkuu wa mpito Abdulhamid Dbeibah

https://p.dw.com/p/46plt
Libyen | Fathi Bashagha kandidiert als Präsident
Picha: Hazem Turkia/AA/picture alliance

Msemaji wa bunge hilo Abdullah Bliheg amesema kupitia ukurasa wa twitter kwamba baraza la wawakilishi limemuidhinisha Bashagha kuongoza serikali, baada ya mpinzani wake kujiondoa, ingawa haikuweka wazi iwapo wabunge walipiga kura.

Dbeibah aliye madarakani amekwishasema kwamba halitambui jaribio la bunge la kumuondoa, na kwa maana hiyo serikali itaendelea kutambulika na hatajiuzulu huku akiapa kwamba atakabidhi madaraka kwa serikali pekee itakayochaguliwa.

Waziri Mkuu huyo wa mpito alinusurika katika jaribio la mauaji mapema  wakati gari lake liliposhambuliwa kwa risase saa chache kabla ya kura ya wabunge, lakini hakuna taarifa rasmi iliyotolewa ili kuthibitisha hilo.

Bunge linalenga kuchukua udhibiti wa mustakabali wa kisiasa wa Libya baada ya kusambaratika kwa mchakato wa uchaguzi ulipangwa kufanyika Disemba, na kutaja kuwa serikali ya mpito ya Dbeibah si halali tena.

Wachambuzi wahofia mzozano zaidi Libya 

Ägypten Kairo | Libyscher Premierminister Abdul Hamid Mohammed Dbeibah
Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid Mohammed DbeibahPicha: Hazem Ahmed/AP Photo/picture alliance

Wachambuzi wanasema matokeo ya hatua za alhamisi hii yanaweza kurejesha kipindi cha mgawanyiko ambacho kilimalizika mwishoni mwa mwezi Machi baada ya uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Dbeibah. Hata baadhi ya wagombea Urais wanaipinga hatua hii, kama alivyosema mgombea Mostafa Al-Majdub.

Hata hivyo, wakati majeshi ya wapinzani yakikusanyika mjini Tripoli katika wiki za hivi karibuni, wachambuzi wanasema hilo halimaanishi kuwa mgogoro huo wa kisiasa utazusha mapigano hivi karibuni.

Mshauri wa Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi kuhusu Libya amesema Serikali ya Dbeibah ya Umoja wa Kitaifa bado ni halali huku akilihimiza bunge kujikita zaidi katika kuandaa uchaguzi ujao.

Takriban Walibya milioni 3 walijiandikisha kupiga kura mwezi Disemba, lakini misuguano ya kisiasa na ucheleweshaji vilivyojitokeza vimewakasirisha na kuwakatisha tamaa wengi wao.

Spika wa Bunge Aguila Saleh amesema wabunge takriban wote wameitikia kikao siku ya Alhamisi, ikiwa ni idadi ya kutosha kwa ajili ya kuidhinisha kura hiyo, huku picha za televisheni zimeonyesha bunge lilojaa.

Kuchaguliwa kwa Bashagha si lazima kusababishe mara moja makabiliano na Waziri Dbeibah kwani inaweza kuchukua muda hadi Bashagha kuunda serikali inayokubalika na pande zote.

Chanzo: RTRE, APE