1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU inadai Uturuki inajihusisha ukiukaji wa haki za binadamu

Faiz Musa14 Machi 2019

Wabunge hao wanadai rais wa Uturuki Tayyib Erdogan amekuwa akijihusisha na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya umoja huo.

https://p.dw.com/p/3F0j6
Europäisches Parlament für Beitrittsverhandlungen mit der Türkei
Picha: picture-alliance/dpa/C. Hartmann

Wabunge katika bunge la Ulaya walipiga kura kwa wingi kulikataa ombi la taifa la Uturuki kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya. Wabunge hao wanadai rais wa Uturuki Tayyib Erdogan amekuwa akijihusisha na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya umoja huo.

Wabunge 370 walipiga kura kulisimamisha ombi hilo la Uturuki dhidi ya wabunge 109 waliopiga kura kutaka Uturuki ikubaliwe kujiunga na umoja wa Ulaya, huku wabuge 143 wakikosa kupiga kura.

Umoja wa Ulaya unasema kwamba Uturuki haiwezi kujiunga na jumuiya hiyo kwa sababu ya kuhujumu uhuru wa watu kuzungumza, wapinzani kuwekwa viuzuizini na ukiukaji wa haki za kimsingi za raia.

Mbunge wa siasa za wastani za mrengo wa kulia kutoka Uholanzi Kati Pir ambaye aliunga mkono kutoruhusiwa kwa uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya amedai Erdogan amekuwa akitumia mabavu katika uongozi wake kwa kuwakamata wapinzani na vile vile kuporomoka kwa uhuru wa mahakama.

Flagge Türkei und EU
Bendera ya Uturuki (kulia) na bendera ya Umoja wa Ulaya (kushoto)Picha: Imago/F. Sorge

Msemaji wa chama kinachotawala  nchini Uturuki AK, Omar Celik amepuzilia mbali matokeo ya kura hiyo akisema hayana maana yoyote na ni batili.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alisema alitarajia wabunge hao watafanya maamuzi ya busara  na kuja na njia nzuri itakayoiwezesha Uturuki kujiunga nao.

Uturuki imekuwa ikitaka kujiunga na EU miongo kadhaa sasa

Bunge hilo la ulaya lina mamlaka ya kuruhusu uanachama wa taifa lolote katika umoja huo.

Miongo kadhaa nyuma Uturuki iliwasilisha ombi lake la kutaka kujiunga rasmi na umoja huo ila mazungumzo juu ya hilo yalianza mwaka 2005.

Mbunge wa siasa za wastani za mrengo wa kulia kutoka Ureno Lilian Rodrigues alisema wanatambua Uturuki imekuwa muhimu sana katika mgogoro wa Syria ila suala hilo haliwezi kuushikilia  mateka Umoja wa Ulaya kuiruhusu nchi hiyo  kujiunga na jumuiya hiyo  kwa kutambua pia Uturuki haitaki maoni tofauti  ya wengine.

Maamuzi ya bunge hilo la Ulaya yamekuja siku mbili kabla ya mwakilishi wa maswala ya kigeni wa umoja huo Federica Mogherini kufanya kikao na waziri wa maswala ya kigeni wa Uturuki mjini Brussels kuhusu uhusiano wa pande hizo mbili.

Siku ya Jumapili waandishi habari wawili wa Ujerumani waliondoka Uturuki baada ya serikali hiyo kukataa kuwapa vibali vya kufanya kazi nchini humo jambo lililokosolewa  na Ujerumani na kusababisha  wasiwasi wa kidiplomasia.

(RTRE)