Bunge la DRC lamuondoa spika | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.12.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Bunge la DRC lamuondoa spika

Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limepiga kura ya kumuondoa spika wa bunge hilo, Jeanine Mabunda, mshirika wa karibu wa rais mstaafu Joseph Kabila.

Wabunge 484 walihudhuria kikao cha jana jioni kujadiliana iwapo wamuondoe Mabunda katika nafasi ya uspika, huku 281 wakipiga kura ya kumfuta kazi na wengine 200 walipinga uamuzi huo. Na hatua ya kuondolewa spika huyo inampa Rais Felix Tshisekedi ushindi mkubwa katika mzozo mkali wa kuwania madaraka kati yake na wafuasi wa Kabila. 

Wabunge wa Kongo wamechukua uamuzi huo baada ya kumshutumu Spika Mabunda kwa kuegemea zaidi kwenye mrengo wa kisiasa katika uongozi wake na kutokuwa muwazi linapokuja suala la kusimamia fedha za bunge hilo. Hata hivyo, spika huyo alikana shutuma zilizotolewa dhidi yake na aliomba radhi kutokana na hali ya kutoelewana iliyojitokeza. Awali, alilisihi bunge kulikataa pendekezo lililowekwa dhidi yake na wafuasi wa Tshisekedi kwa sababu zisizo za kisiasa.

Nguvu kwa washirika wa Tshisekedi

Ushindi huu wa wapinzani wa Kabila ni ishara kubwa ya nguvu ya washirika wa Rais Tshisekedi ambao kwa sasa wanaweza kuwa na wingi wa kutosha ikilinganishwa na baraza la mawaziri ambalo wajumbe wake wengi ni wafuasi wa Kabila. Kura hiyo imepigwa baada ya siku kadhaa za ghasia ndani ya bunge hilo, hatua iliyosababisha polisi kuingilia kati ili kuituliza hali ya mambo.

Soma zaidi: Bunge lafungwa Kongo kutokana na vurugu za kivyama

Wafuasi wa Kabila wa muungano wa kisiasa wa FCC wanamshukutu Tshisekedi kwa kukiuka katiba. Chama hicho kinasema Tshisekedi anapanga njama za kuanzisha utawala wa kidikteta. ''Kila kitu ambacho tumefanya hapa kimekuwa na msingi wa kitapeli. Kwa kweli tulilazimika kulikataa hili ambalo tunaliona hapa na hatukupaswa hata kupiga kura,'' alisema Paulin Kashomba ni mfuasi wa Kabila.

Bildkombo I Félix Tshisekedi und Joseph Kabila

Rais wa DRC, Felix Tshisekedi na rais wa zamani, Joseph kabila

Mfuasi wa Rais Tshisekedi, Jose Ngulamulumbe amesema wanafuraha kwa sababu Jeanine Mabunda ameondolewa katika bunge na kwamba siasa za Kabila sasa hatimaye zinaondoka, kwani wao wanamtaka tu Felix Tshisekedi.

''Kuondoka kwa Spika Mabunda ni kuondoka kwa Kabila na ndiyo mwisho wa utawala wa Kabila,'' alifafanua Ngulamulumbe.

Mwanadiplomasia mmoja amesema kuwa nafasi kati ya wafuasi wa Tshisekedi na Kabila zinaonekana hazina upatanisho na ni vita kati ya pande hizo mbili. Anasema anahofia kuhusu kuzuka kwa mivutano mikubwa katika taasisi za kisiasa za Kongo.

Mamia ya polisi walidhibiti eneo la kuingilia katika bunge hilo na kuwaruhusu tu wabunge na waandishi habari wenye vibali maalum na wafanyakazi wa bunge kuingia ndani.

Baada ya takriban miaka miwili ya kujaribu kuepukana na mamlaka ya Kabila, mwezi uliopita Tshisekedi alianzisha mazungumzo na viongozi wa kisiasa, kidini na vyama vya kiraia. Aidha, Jumapili iliyopita, rais huyo wa Kongo alitangaza kuuvunja ushirikiano na muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Kabila, FCC, ambavyo vina wingi wa viti bungeni.

(AFP, Reuters)