1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

200110 Angola Verfassung

Josephat Nyiro Charo21 Januari 2010

Rais José Eduardo dos Santos aimarisha mamlaka yake

https://p.dw.com/p/LcRw
Rais wa Angola Jose Eduardo dos SantosPicha: AP

Kwa kawaida timu za mpira wa miguu hufanya kila juhudi kuepukana na kuongezewa muda wa ziada wakati wa michuano. Katika siasa, lakini, hali ni tofauti kabisa - wanasiasa wengi wanajaribu kurefusha muda wao wa kukaa madarakani kwa vipindi virefu kadri inavyowezekana. Bingwa katika fani hii ni rais wa Angola, José Eduarado dos Santos, ambaye amekuwa akiitawala nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 30. Sasa, kiongozi huyo anataka kuibadili katiba ili aendelee kubakia madarakani hata baada ya kuahidi kuandaa uchaguzi nchini Angola.

Huku Waangola wakifurahia kuingia katika robo fainali kwenye michuano ya kuwania kombe la Afrika inayoendelea nchini mwao, leo bunge la nchi hiyo linapiga kura kuidhinisha katiba mpya ambayo itabadili mfumo mzima wa kisiasa wa nchi hiyo. Angola na Algeria zilitoka sare bila kufungana wakati wa mchuano uliochezwa siku ya Jumatatu wiki hii.

Rais wa Angola José Eduardo dos Santos alifurahishwa sana na ufanisi wa timu ya Angola katika michuano hiyo, lakini leo, kupitia bunge, anataka kuibadili katiba ya nchi bila katiba hiyo kujadiliwa hadharani. Raul Danda, wakili anayepigania haki za raia, ni mbunge aliyechaguliwa kupitia chama kikubwa cha upinzani nchini Angola, UNITA. Anakosoa hatua inayochukliwa na rais Santos.

"Katiba ni sheria msingi ambazo sharti zijadiliwe kwa kina. Haiwezekani kufanya hivyo haraka haraka. Mjadala kuhusu katiba ulitakiwa uendelee hadi mwezi Aprili au Mei mwaka huu, lakini tayari umemalizika. Katiba haitajadiliwa hadharani tena kama ilivyokuwa imepangwa, na kama jumuiya ya kiraia ilivyotarajia. Katiba sasa itapigiwa kura moja kwa moja na bunge."

Zoezi la kuipigia kura katiba bungeni hii leo inafanyika tu kuficha kombe ili mwanaharamu apite, lakini matokeo yanajulikana. Vyama vya upinzani nchini Angola vikiwemo chama cha UNITA, FNLA na PRS vimepinga hadharani katiba hiyo mpya, lakini havina mabavu ya kushindana na chama tawala cha MPLA ambacho kina wabunge 191 kati ya wabunge wote 220 katika bunge la Angola.

Upinzani unaikosoa katiba mpya, ukisema uchaguzi wa moja kwa moja wa rais utafutwa. Katika siku za usoni uchaguzi wa bunge utaendelea kufanyika. Rais wa Angola atakuwa kiongozi wa chama kitakachopata idadi kubwa ya kura.

Katiba mpya ya Angola inayopigiwa kura na bunge hii leo itaanza kufanya kazi ifikapo mwaka 2012. Hadi wakati huo, rais wa sasa, José Eduardo dos Santos, ataendelea kuitawala nchi hiyo. Emanuel Lopes, mtaalam wa sayansi katika taasisi ya utafiti ya Afrika mjini Lisbon, nchini Ureno, anasema rais Santos atakuwa akiitawala Angola bila kibali cha wananchi ambao wana haki, kidemokrasia, kumchagua kiongozi wamtakaye.

"Kuna katiba halali iliyopitishwa mnamo mwaka 1992 inayosema rais anatakiwa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi katika uchaguzi mkuu. Kinachoendelea hivi sasa si halali na uvunjaji wa katiba iliyopo."

Kupitia katiba mpya, rais José Edaurdo dos Santos atazidi kuimarisha mamlaka yake. Yeye sio tu kiongozi aliyekaa madarakani kwa kipindi kirefu zaidi duniani, bali pia familia yake inamiliki kampuni zote kubwa kubwa nchini Angola. Kutokana na utajiri wake wa mafuta, Angola ni nchi ya tatu tajiri barani Afrika. Mengi hayajulikani kuhusu biashara za familia ya rais Santos nchini Angola.

Upinzani nchini Angola unataka kuizuia katiba mpya kupitia mahakama za nchi hiyo, lakini inahofiwa hakutapatikana ufanisi wowote, kwani rais José Eduaurdo dos Santos anaidhibiti nchi.

Mwandishi:Beck, Johannes/Josephat Charo/ZPR

Mhariri: Othman Miraji