1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kupambana na IS

30 Januari 2015

Ujerumani inapanga kuitika wito wa wanamgambo wa kikurd Peshmerga na kutuma silaha zaidi na vipuri kaskazini ya Iraq mwezi ujao wa februari

https://p.dw.com/p/1ETJM
Bunge la shirikisho BundestagPicha: picture-alliance/AP Photo/Michael Sohn

Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen amedokeza katika mahojiano na kituo cha televisheni kwamba mitambo ya kufyetulia makombora chapa "Milan" ni sehemu ya shehena mpya ya silaha watakazopelekewa wanamgambo wa kikurd Peshmerga. Hadi sasa jeshi la shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Bundeswehr limeshatuma mitambo 30 na makombora 500 ya aina hiyo.Waziri von der Leyen ameongeza kusema silaha hizo zenye uwezo wa kuhujumu vifaru zinaweza kutumiwa na wanamgambo wa Peschmerga kushambulia magari makubwa makubwa yanayosheheni mabomu ya waasi wa dola ya kiislam IS.

Mpango huo wa kutumwa silaha umeidhinishwa na bunge la shirikisho Bundestag kutokana na wingi wa kura za wabunge wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano mjini Berlin.

Jeshi la shirikisho Bundeswehr limeshawapatia Peschmerga silaha zenye thamani ya Euro milioni 70 kutoka shehena yake wenyewe.

Waziri von der Leyen aliahidi misaada ziada kwa Peschmerga alipoitembelea Iraq wiki mbili zilizopita:"Perschmerga kimsingi hawana chochote,ndio maana tumeamua kujizatiti.Kwa mfano nguo za msimu wa baridi,huduma za afya jambo ambalo ni muhimu kabisa.Lakini silaha na vipuri,tutajaribu hivi sasa kupata ridhaa ya serikali kuu. Nnaweza kukadiria hadi mwisho wa mwezi wa february tutakuwa tumeshakamilisha kila kitu kuweza kutuma silaha na vipuri."

Wanajeshi wa Ujerumani kuwapatia mafunzo Peschmerga

Mbali na silaha serikali ya Ujerumani inapanga pia kuwapeleka hadi wanajeshi 100 kutoa mafunzo kaskazini ya Iraq.Watawapatia mafunzo ya kijeshi wanamgambo wa Perschmerga katika mapambano yao dhidi ya wafuasi wa dola ya kiislam IS.Wanajeshi hao watawekwa katika mji wa Erbil.Wanajeshi hao wa Ujerumani hawatakuwa na jukumu la kupigana hata hivyo watakuwa na silaha ili waweze kujihami.

Ursula von der Leyen bei Erbil 12.01.2015
Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen akiamkiana na wanajeshi wa kike wa kikurd,huko Erbil nchini IraqPicha: Reuters/M. Gambarini

Die Linke wanapinga mpango huo

Mipango yote miwili,tangu ule wa kuwapatia silaha mpaka huu wa kuwapatia mafunzo ya kijeshi Peschmerga,inazusha mabishano humu nchini.Upande wa upinzani wa mrengo wa kushoto die Linke unahisi kuna njia bora zaidi za kupambana na wafuasi wa itikadi kali wa IS.Njia zao za kujikusanyia fedha zinaweza kufungwa kwa mfano na kuzuwiliwa mikururo ya wanampango wanaopitia Uturuki kuingia Iraq.

Kurden drängen IS im Sinjar-Gebirge zurück 18.12.2014
Wanamgambo wa kikurd PeschmergaPicha: Reuters/A. Jalal

Mwandishi:Gräßler,Bernd/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Yusuf Saumu