Bundesliga:Bochum yamtimua kocha wake | Michezo | DW | 21.09.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bundesliga:Bochum yamtimua kocha wake

FC Cologne mwishoe yashinda !

default

Marcel Koller atimuliwa Bochum.

Haile Gebrselassie wa Ethiopia,anyakua ushindi wa 4 mfululizo wa Berlin marathon,lakini mara hii, bila ya kuvunja rekodi yake ya dunia.

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, inajaza nafasi ya mwisho ya nusu-finali ya kombe la klabu bingwa barani Afrika-champions-league.

Katika Bundesliga-Bochum yametimua kocha wake Marcel Koller wakati FC Cologne ikijiwinda kwa changamoto ya keshokutwa ya Kombe la Shirikisho na mabingwa Wolfsburg,watoroka na ushindi wao wa kwanza msimu huu huko Stottgart.

Katika Kombe la Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB Pokale) Jumatano hii kwa jicho la changamoto za mwishoni mwa wiki za Bundesliga-Ligi ya Ujerumani,

VFL Bochum ,itatarajia kufungua ukurasa mpya Jumatano hii itakapoingia uwanjani na mahasimu wao wa mtaani Schalke 04 kwa mpambano wa kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani .Hii ni baada ya mwishoni mwa wiki kuzabwa mabao 3-2 na Mainz.

Pigo hilo nyumbani, lilizusha hasira kwa mashabiki na hii jana ikaongoza kutimuliwa kwa kocha Marcel Kohller kutoka Uswisi.Nafasi yake sasa inachukuliwa na chipukizi 2 katika fani hiyo, msaidizi wa hadi sasa wa kocha Koller , Frank Heinemann na stadi wa zamani wa Bochum, Dariusz Wosz.

Na hivi ndivyo tangazo la kumtimua Marcel Koller,mswisi mwenye umri wa miaka 48 lilivyotolewa huko Bochum:

"Tumeachana mkono leo na kocha Marcel Koller.Kuanzia kesho Frank Heinemann na Darius Wösch, watashika uongozi wa ukocha."

Bochum chini ya uongozi mpya ina miadi kwa changamoto yake ya kwanza na Schalke keshokutwa Jumatano. Timu nyengine iliokumbwa na msukosuko ni Hertha Kocha wake pia mswisi Lucien Favre, yumo pia mashakani. Baada ya kujikuta sasa inaburura mkia wa Bundesliga-Berlin, inahitaji ushindi Jumatano hii ili kurejesha imani katika kikosi chake na kwa mashabiki wa jiji kuu la Ujerumani. Berlin ilizabwa mabao 4:0 na Freiburg -timu iliopanda daraja ya kwanza msimu huu.

Mabingwa mara kadhaa wa Bundesliga-Bayern Munich wanaokumbana kesho na Rot-weiss Oberhausen katika Allianz Arena,walitamba kwa mabao 2-1 mbele ya Nuremberg.Kesho wanatazamia kumteremsha tena mshambulizi wao aliekua ameumia, mtaliana Luca Toni.Jumamosi ijayo watabidi kujiwinda watakapoitembelea Hamburg iliopo kileleni mwa Ligi.

Mwishoe, FC Cologne imejikomboa mkiani mwa Ligi ilipoisangaza Stuttgart Jumamosi kwa mabao 2:0 mjini Stuttgart. Sasa Cologne haiko tena katika safu ya timu zinazoweza kuteremshwa daraja ya pilialao kwa sasa. Jumatano Cologne inacheza na mabingwa Wolfsburg.

Katika Premier-League-Ligi ya Uingereza , Chelsea imesalia kileleni ikiongoza kwa pointi 3.Katika changamoto ya mahasimu 2 wa mtaani Manchester United na Manchester city ,Manu ilitokwa na jasho hadi dakika ya mwisho ya kufidia kuwazima city kwa mabao 4-3.Kocha wa Manu Sir Alex Ferguson aliuleza mpambano huo kuwa changamoto kali kabisa ya timu hizo 2 za mtaani ya muda wote.

Katika kinyanganyiro cha kombe la klabu bingwa barani Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, inajaza nafasi ya mwisho ya timu za nusu-finali ya Kombe hilo mwaka huu:

Simba wa Lumbubashi, jana walinguruma mtaani na Etoile du sahel waliondoka bila ya pointi kurudi Tunisia. Beki wao mshahara Kanyimbo Tshizeu aliwaimbia kweli nyimbo mabingwa hao wa zamani wa Afrika kwa bao lake la dakika ya 35 ya mchezo nyumbani Lumbubashi.

Ushindi huo sasa umeipatia TP mazembe tiketi ya nusu-finali kati yake na Al-Hilal ya Sudan.Etoile ambayo iliwasangaza mabingwa mara 6 wa Afrika Al Ahly ya Misri kwa kuwachapa mabao 3-1 mjini Cairo miaka 2 iliopita na kutwaa ubingwa wa Kombe hili, imemaliza nafasi ya 3 wakiwa na pointi 7-moja zaidi kuliko wazimbabwe Monomotapa.

Nusu-finali ya pili mwezi ujao , itakua kati ya timu 2 za Nigeria wenyewe kwa wenyewe :Kano Pillars na Heartland. Timu gani 2 zitaumana katika finali ya mwaka huu ,tutajua baada ya nusu-finali hizo. Simba wa lumbubashi wanadai huu ni mwaka wao tena kunguruma baada ya kuwa timu ya kwanza kabisa ya Afrika kutwaa Kombe hilo mara 2 mfululizo.

Berlin -maraton:

Mzee Gebrselassie wa Ethiopia, ambae mwezi uliopita alikataa kushiriki katika mbio za marathon za ubingwa wa dunia,jana alitamba tena mjini Berlin alipotoroka na ushindi mwengine-wanne mfululizo wa Berlin marathon.

Gebrselassie, alishinda jana Berlin- marathon kwa mwaka wa 4 mfululizo.Mara hii lakini, bila ya kuweka rekodi ya dunia.Muda wake wa ushindi, ulikuwa masaa 2, dakika 6 na sek.8.Muda huo , ni nje kabisa ya rekodi yake ya dunia ya masaa 2, sek.03 nukta 59 alioiweka mjini Berlin mwaka jana.Mkenya Francis Kiprop,alikuja wapili nyuma ya Selassie na muethiopia Negari terfa alifuata nafasi ya tatu.

"Kasi niliotia ilikuwa safi kabisa .Kwani, nilikua katika mwendo wa kuvunja rekodi hadi tulipofikia km 33." Alisema Gebrselassie alieweka rekodi isio rasmi ya km 30 kwa muda wa saa 1,dakika 27 na nukta 49."Nikijihisi fit kabisa hadi hapo, halafu lakini nikaanza kuhisi joto na hapo nikapotea njia."-aliongeza Gebrselassie huku akitabasamu.

Akitoa shukurani zake za dhati kwa wajerumani kwa jumla na kwa wakaazi wa Berlin hasa: Gebrselassie alisema:

"Ni tukeo la kuvutia sana na shukurani nyingi kwa wajerumani na hasa kwa wakaazi wa Berlin ambao wamefanya kazi nzuri."

Gebrselassie, ametawazwa mara mbili bingwa wa olimpik wa mbio za mita 10.000 na ameshinda mara 4 mfululizo taji la ubingwa wa riadha duniani-world athletics championsship- katika masafa hayo.Upande wa wanawake, ushindi pia ulienda kwa Ethiopia. Atsede Habtamu Besuye alitimka mbio na kushinda kwa muda wa masaa 2, dakika 24 na sek.

Muandishi:Ramadhan Ali /AFP/RTRE

Mhariri: M.Abdul-Rahman