1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yarejea uwanjani

Admin.WagnerD17 Januari 2013

Ligi ya soka ya Ujerumani, Bundeliga, inarejea tena dimbani (terehe 18 Januari)baada ya mapumziko ya majira ya baridi kwa msimu wa mwaka 2012/2013.

https://p.dw.com/p/17Ltj
Am 29. Spieltag der Fußball-Bundesliga Saison 1991-1992 stehen sich in Frankfurt Eintracht Frankfurt und der FC Bayern München gegenüber. Die Eintracht gewann das Spiel mit 3:2. Der Frankfurter Anthony Yeboah versucht sich gegen Münchens Verteidiger Thomas Berthold durchzusetzen.
Fußball Bundesliga Anthony Yeboah Eintracht FrankfurtPicha: picture-alliance/dpa

Mengi yanatarajiwa katika kipindi hiki baada ya awamu iliyopita kukumbwa na timuatimua ya makocha kutokana na matokeo mabaya ya baadhi ya vilabu vinavyoshiriki kinyang'anyiro hicho.

Ijumaa (tarehe 18 Januari) Bundesliga itaanza kwa klabu ya soka ya Schalke kushikana mashati na Hannover katika mechi itakayochezwa usiku saa moja na nusu kwa saa za hapa Ujerumani ambazo ni sawa na saa 3 na nusu Afrika ya Mashariki.

Mchezaji wa Hannover Didier Ya Konan.
Mchezaji wa Hannover Didier Ya Konan.Picha: Getty Images/AFP

Vinara wa Bundesliga, Bayern Munich, wataumana na Greuther Fuerth Jumamosi (19.1.2013) huku wakiwa na matumaini ya kuwa na mwanzo mzuri wa awamu hii.

Matumaini ya Bayern Munich

Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, mwenye umri wa miaka 67 sasa, ana mategemeo ya kustaafu vyema hapo mwenzi Mei mwaka huu kwa kukiwezesha kikosi chake kunyakua taji la Bundesliga msimu huu.

Heynckes atarithiwa na mkufunzi machachari wa kabumbu la kimataifa kutoka klabu ya Barcelona, Pep Guardiola, ambaye tayari Bayern Munich imeshaweka wazi kuwa kocha huyo ni wao katika msimu ujao.

Pep Guardiola, Kocha mpya wa Bayern Munich 2013/2014
Pep Guardiola, Kocha mpya wa Bayern Munich 2013/2014Picha: AP

Wana Bavaria hao wenye jumla ya pointi 42, wako kileleni kwa tofauti ya pointi tisa kutoka nafasi ya pili inayoshikiliwa na Bayer Leverkusen yenye pointi 33 huku mabingwa watetezi wa taji la Bundesliga msimu uliopita, Borussia Dortmund, wakishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 30.

Leverkusen, ambao walimaliza ngwe iliyopita mwezi Desemba mwaka jana kwa kushinda mechi tano kati ya sita walizocheza, kesho watachuana na Eintracht Frankfurt wanaoshikilia nafasi ya nne. Frankfurt kama walivyo Dortmund nao pia wana jumla ya pointi 30 huku taarifa zikisema kuwa sasa mshambuliaji wao machachari, Stefan Kiessling, akiwa ameiva vyema kwa ajili ya ngwe hii.

Ndoto za Dortmund kutetea taji lake

Kwa upande wao Borussia Dortmund wanaopigana kufa na kupona kulinda taji la Bundesliga Jumamosi (19.1.2013) watasafiri kwenda kukutana na Werder Bremen katika mchezo ambao unategemewa kuweza kuinua matumaini ya wapenzi wa mabingwa hao watetezi.

Tunafahamu mabadiliko kadhaa yalifanyika katika Bundesliga kabla ya mapumziko ya majira ya baridi ambapo tumeshuhudia baadhi ya vilabu vikiwatimua makocha wake kutokana na matokeo mabaya katika kinyang'anyiro hicho.

Baadhi ya wachezaji wa Borussia Dortmund wakiwa mazoezini
Baadhi ya wachezaji wa Borussia Dortmund wakiwa mazoeziniPicha: Getty Images

Na katika ngwe hii kila timu imetangaza kufanya maajabu ya kuwania taji. Bila shaka kuna mengi ya kushuhudiwa katika Bundeliga hasa wakati huu wachezaji wamerudi na nguvu mpya kabisa baada ya mapumziko.

Mechi zingine zitakazochezwa Jumamosi ni Mainz ambao watachuana na Freiburg, Wolfsburg wataumana na Stuttgart na Hoffeinheim itakwaana na Moenchengladbach.Jumapili kutakuwa na michezo miwili ambapo Nuremberg itacheza na Hamburg wakati Fortuna Dusseldorf itakutana na Augsburg.

Mwandishi: Stumai George/Dpa/Reuters/Afp

Mhariri: Josephat Charo