1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yafikia tamati wikendi hii

Admin.WagnerD22 Mei 2015

Mchezo wa 34 wa mwisho katika Bundesliga msimu huu jioni ya leo utakuwa burudani kwa wapenzi wa kandanda wakishuhudia timu sita zikijaribu bahati yao kusalia katika ligi daraja la kwanza.

https://p.dw.com/p/1FURM
Deutschland Klopp und Guradiola
Picha: imago/Ulmer

Kocha wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp anapanga kuhitimisha mchezo wake wa mwisho katika Bundesliga kama kocha wa timu hiyo nyumbani kwa ushindi dhidi ya Werder Bremen.

Baada ya kupata mataji mawili ya ligi ya Ujerumani Bundesliga pamoja na kucheza katika fainali ya kombe la Champions League katika muda wa misimu saba akiwa na Borussia Dortmund kocha Jurgen Klopp ataiongoza timu hiyo kwa mara ya mwisho leo jioni katika uwanja wa Westfalen na anataka kikosi chake kuonesha mchezo wa hali ya juu kabisa. "Ni matumaini yangu kwamba tutaonesha mchezo wa hali ya juu wa Dortmund na kuonesha tukio la hali ya juu," alisema Klopp ambaye nafasi yake itachukuliwa na Thomas Tuchel msimu ujao.

Deutschland 2. Fußball Bundesliga FC Ingolstadt vs. RB Leipzig
Klabu ndogo ya Ingolstadt wamepandishwa darajaPicha: Getty Images/A. Pretty

Mchezo wa mwisho wa kocha huyo mwenye umri wa miaka 47 akiwa katika benchi la ufundi la Borussia Dortmund , ni katika uwanja wa Olimpiki mjini Berlin katika fainali ya kombe la Ujerumani DFB Pokal , dhidi ya Wolfsburg hapo Mei 30, lakini anataka kushinda dhidi ya Bremen ili kumaliza katika nafasi ya sita.

Bremen ikiwa katika nafasi ya nane na Dortmund ya saba , zinahitaji pointi tatu, na kutarajia kwamba Borussia Moenchengladbach itashinda dhidi ya Augsburg , na zinaweza timu hizo mbili kumaliza katika nafasi ya sita na kujihakikishia nafasi ya kucheza katika ligi ya Europa , Europa League msimu ujao.

Bayern Munich watatawazwa mabingwa wa ligi ya Ujerumani leo jioni kwa mara ya 25 bila kujali matokeo ya mchezo wao nyumbani dhidi ya Mainz 05. Kikosi cha Pep Guardiola kinaonekana kitakamilisha mchezo huu wa mwisho kwa ushindi baada ya kupata vipigo mfululizo katika michezo sake mitano kati ya sita.

Waliondolewa katika kinyang'anyiro cha Champions League na kombe la Ujerumani , DFB Pokal katika nusu fainali katika wiki nne zilizokuwa za majonzi mno kwa timu hiyo tangu kushinda ubingwa wa ligi wakati zimebakia mechi nne ligi kumalizika. Lakini Guardiola ameshinda mataji matano katika muda wa miaka miwili akiwa na kikosi hicho cha Bayern.

Deutschland fußball Trainer FC Bayern München Josep Guardiola
Kocha wa Bayern Pep GuardiolaPicha: Getty Images/Bongarts/D. Grombkowski

Moja katika mapambano makali kabisa ya kuepuka kushuka daraja katika historia ya Bundesliga yatashuhudiwa leo wakati timu sita za chini zikiwania kuepuka kushuka daraja.

Timu mbili za chini kabisa , kwa sasa Paderborn na Hamburg SV, zitashuka moja kwa moja kwa kuwa timu iliyoko katika nafasi ya 16, nafasi tatu kutoka chini itacheza na timu bora ya tatu katika daraja la pili na kuaamua ipi ishuke kati ya hizo.

Parderborn haiwezi kupanda zaidi ya namba 16, hali itakayowapa nafasi ya kuendelea kuishi katika daraja la kwanza kwa kucheza mchezo huo dhidi ya tumu iliyoko katika nafasi ya tatu katika daraja la pili. Lakini Paderborn inakwaana jioni ya leo na Stuttgart , timu iliyoko nafasi mbili tu juu yake, wakati timu inayowatewnganisha Hamburg iko nyumbani ikipambana na Schalke 04 iliyoko katika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi.

Hamburg timu pekee katika ligi ya Ujerumani ambayo haijawahi kushuka daraja , itakosa huduma ya mchezaji wake wa kati Marcell Jansen ambaye ana maumivu katika paja.

Hannover iko nyumbani kwa Freiburg, ambayo ilipata ushindi wa kushangaza wa mabao 2-1 dhidi ya mabingwa Bayern Munich Jumamosi iliyopita, ambapo timu zote hizo mbili zina pointi 34, pointi moja tu juu ya nafasi za kushuka daraja, hii ina maana hakuna timu inayoweza kubweteka na kuachia hata pointi moja. Hertha Berlin inaweza kuporomoka kutoka nafasi ya 13 na kutumbukia katika zoni ya kushuka daraja hadi nafasi ya 16 iwapo itashindwa na Hoffenheim na kuingia katika hatari ya kushuka kwa mara ya tatu katika muda wa miaka mitano.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Khelef