1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga mapumzikoni, RB Leipzig mabingwa duru ya kwanza

Sekione Kitojo
23 Desemba 2019

Ligi ya  Ujerumani Bundesliga yaingia  mapumziko, wakati RB Leipzig kwa mara ya kwanza ni bingwa wa mzunguko wa kwanza, bingwa wa majira ya  mapukutiko.

https://p.dw.com/p/3VHJ8
Fußball Bundesliga RB Leipzig vs. FC Augsburg
Picha: AFP/R. Hartmann

RB Leipzig  imekaa  kileleni mwa  msimamo  wa  ligi  ya  Ujerumani , Bundesliga , wakati  ligi  hiyo  ikienda mapumziko  ya  majira  ya baridi na  sikukuu  ya  Krismas, ikiiondoa Borussia Moenchengladbach  iliyokuwa  katika  nafasi  hiyo  kwa  muda  mrefu wa  sehemu  hii  ya  kwanza  ya  michezo 17  ya  ligi.

RB Leipzig ina pointi 37, ikiipita  Gladbach  kwa  pointi 2, wakati mabingwa watetezi Bayern Munich  wako  nafasi ya  tatu  wakiwa  na  pointi 33. makamu bingwa  Borussia  Dortmund imeshindwa  kusogea  katika  nafasi  ya tatu  baada  ya  kupata  kipigo  bila  kutegemea  cha  mabao 2-1 dhidi  ya  TSG Hoffenheim siku  ya  Ijumaa. Dortmund iko  nafasi  ya 4 ikiwa  na  pointi 30. Kocha  wa  RB Leipzig Julian Nagelsmann ameimwagia  sifa timu  yake kwa  kuwa  mabingwa wa  majira  ya mapukutiko.

Leipzigs Trainer Julian Nagelsmann
Kocha wa RB Leipzig Julian Nagelsmann akifurahia ushindi wa timu yakePicha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

"Tumo katika  mashindano  yote, tumepata  matokeo  mazuri  katika bundesliga. Nafurahia kwa  hilo, ambapo tunapata  muda  kidogo  wa kupumua. Nafurahi  lakini  pia , hapo Januari 6  kila  kitu kinaanza upya  kwa  mazowezi  na  iwapo tunaweza  kujiongeza  zaidi kidogo. Sisi  pia  tunapaswa  kufanya  hivyo. Tuna  uwezo wa  kutosha katika  kikosi  chetu, na hii  ni  safi kabisa. Na  wakati mzunguko wa pili utakwenda  vizuri  kama  duru  hii , tunaweza  bila  shaka  kufanya vizuri."

Schalke 04 imemaliza  mzunguko  huu kwa  kukaa  karibu  na  hasimu wake  mkubwa  Borussia  Dortmund , timu  hizo  hizo  zikiwa  na pointi 30 katika  nafasi  ya  4 na  5.  Timu  iliyopata  mafanikio makubwa  katika  michezo  ya  mwisho  ya  duru  hii  ni  FC Koln ambayo  chini  ya  kocha  wake  mpya Markus Gisdol  imefanikiwa kupata  pointi 9 katika  michezo mitatu ya  mwisho. Huyu  hapa kocha wa  FC Koln  Markus Gisdol.

Fußball   Bundesliga TSG 1899 Hoffenheim vs. BVB Borussia Dortmund
Mchezaji Julian Weigel wa Borussia (kulia) akipambana na Christoph Baumgartner wa TSG Hoffenheim katika pambano lililoishia kwa Hoffenheim kupata ushindi wa mabao 2-1 Picha: Getty Images/C. Kaspar-Bartke

"Iwapo tungefikiri , kwamba tungeweza  kupata  pointi tisa katika  wiki hii ya michezo ya kila baada ya siku tatu, dhidi ya  timu ambazo tumecheza  nazo, bila  shaka  tungesema, kwamba tumeonesha ujasiri  mkubwa. Lakini  kwa  kweli tunafuraha  nyingi. Sasa tunaweza kusherehekea krismas. Lakini bila shaka  hapo mbeleni hatuwezi kushinda michezo yote. Hakuna sababu kwa  mtu hapa Koln kuanza kuota. lakini  kutokana  na  jinsi  tulivyocheza, tunaweza  kujenga  juu ya  msingi  huo."

FC Koln imechupa  kutoka  nafasi  ya  mwisho  ya  ligi hadi  nafasi ya 15, ikiwa  na  pointi 17, ikifuatiwa  na  Fortuna  Dusseldorf yenye pointi 15, Werder Bremen yenye  pointi 14 na  ya  mwisho inayoshikilia  mkia  ni SC Paderborn iliyosalia  na  pointi 12 licha  ya kupata  ushindi w  mabao 2-1 dhidi  ya  Eintracht Frankfurt katika mchezo  wa  mwisho  wa  duru  ya  kwanza.

Fußball Bundesliga 1.FC Köln v Werder Bremen Torjubel 1:0
Wachezaji wa FC Koln wakifurahia bao alilofunga Jon Cordoba namba 15 dhidi ya Werder BremenPicha: Imago Images/Beautiful Sports/A. Kohri

Wakati  huo  huo mchezaji  wa  Bayern Munich Javi Martinez anakabiliwa  na  karibu  wiki  6 nje  ya  uwanja baada  ya  kupata maumivu  ya  misuli katika  mchezo  wa  Jumamosi  ambapo  timu hiyo ilipata  ushindi  wa  mabao 2-0 dhidi  ya  VFL Wolfsburg, amesema  kocha  wa  muda  wa  timu  hiyo Hansi Flick.