Buhari: Nigeria iko tayari kuzungumza na Boko Haram | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Buhari: Nigeria iko tayari kuzungumza na Boko Haram

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, amesema serikali yake iko tayari kuzungumza na wanamgambo wa Boko Haram ili kuwaachia huru wanafunzi wa kike 209 waliowateka nyara mwezi Aprili 2014, kwenye mji wa Chibok.

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari

Akizungumza jana (30.12.2015) na waandishi wa habari, Rais Buhari amesema wamejiandaa kuzungumza na Boko Haram ili kuwaachia huru wasichana hao waliotekwa mwaka uliopita kwenye mji huo wa kaskazini mashariki, kitendo kilichozuwa lawama kali ulimwenguni na wito wa kuachiwa kwao.

''Bado tumeweka wazi msimamo wetu kwamba kama Boko Haram watatuonyesha uongozi wenye kuaminika na wanatuambia wasichana wale wako wapi, basi tumejiandaa kuzungumza nao bila ya masharti yoyote ya awali,'' alisema Buhari.

Buhari amesema hakuna taarifa madhubuti za kijasusi kuhusu mahali waliko wasichana hao, wala namna afya zao zilivyo na hivyo mazungumzo hayo yanaweza yakaanza tu iwapo maafisa wa Nigeria watathibitisha kuwa wasichana hao wako hai. Ameongeza kusema kuwa wanataka kupata uhakika kwamba wasichana hao wako salama.

Wanamgambo wa Boko Haram

Wanamgambo wa Boko Haram

Majaribio kama hayo yalishindikana katika utawala uliopita wa Rais Goodluck Jonathan kwa sababu maafisa walikuwa wanazungumza na watu wasio sahihi, lakini Buhari amesema suala la wasichana wa Chibok bado liko kwenye akili za Wanigeria na serikali yao.

Baadhi ya viongozi wa Chibok wiki iliyopita walisema Rais Buhari amewasahau wasichana hao, kwa sababu alitangaza kwamba jeshi la Nigeria limeshinda kiufundi vita dhidi ya Boko Haram. Lakini mashambulizi 48 ya kundi hilo kaskazini mashariki mwa Nigeria, yaliyosababisha vifo vya watu 50, yamefifisha kauli hiyo ya Buhari.

Wasichana wapatao 200 hawajulikani walipo

Wanafunzi wa kike 276 walitekwa nyara na Boko Haram, lakini wasichana kadhaa walifanikiwa kutoroka muda mfupi baada ya kutekwa. Hata hivyo kiasi ya wasichana 200 hawajulikani walipo na hawajaonekana tangu video yao ilipoonyeshwa mwezi Mei mwaka 2014.

Mamia ya watu wanaoshikiliwa mateka na Boko Haram, waliachiwa huru katika miezi ya hivi karibuni, lakini hakuna msichana hata mmoja kutoka shule ya Chibok, ambaye alikuwa miongoni mwa walioachiwa huru.

Wasichana waliotekwa wa Chibok

Wasichana waliotekwa wa Chibok

Buhari amegusia kwamba anaweza kupiga marufuku uvaaji wa Hijab au vitambaa vingine vya kufunika kichwa kwa wanawake wa Kiislamu, kama wanamgambo wataendelea kuwatumia wanawake waliovaa baibui kufanya mashambulizi ya kujitoa muhanga.

Boko Haram inawashikilia maelfu ya watu na wiki mbili zilizopita jeshi lilisema lina taarifa za kijasusi kwamba wanamgambo hao wenye itikadi kali wanapanga kufanya utekaji mwingine wa umma.

Zaidi ya watu 17,000 wameuawa katika mashambulizi ya kundi la Boko Haram yaliyofanywa katika kipindi cha miaka sita, ambalo linataka kuunda taifa huru la Kiislamu kwenye nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Wakati huo huo, Rais Buhari mwenye umri wa miaka 73, amesema serikali yake inafanya vizuri sana katika mapambano dhidi ya rushwa, moja ya suala la msingi katika utawala wake. Ameapa kuwa hakuna mtu yeyote, wakiwemo mawaziri wake ambao watasalimika katika kampeni yake ya kupambana na rushwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com