Buhari ashinda uchaguzi wa rais Nigeria | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Buhari ashinda uchaguzi wa rais Nigeria

Muhammadu Buhari ametangazwa mshindi katika kinyang'anyiro cha urais nchini Nigeria mwaka 2015. Mpinzani wake wa karibu, rais wa sasa Goodluck Jonathan amekubali kushindwa na kumpongeza mshindi.

Muhammadu Buhari, rais mteule wa Nigeria.

Muhammadu Buhari, rais mteule wa Nigeria.

Matokeo ya mwisho baada ya kuhesabu idadi kubwa ya kura yalimpa mgombea wa upinzani Muhammadu Buhari kura milioni 15.4, dhidi ya milioni 13.3 za rais Jonathan. Hilo lilikuwa pengo kubwa ambalo asingeweza kuliziba kwa kura zilizobakia.

Rais wa sasa Goodluck Jonathan alimpigia kura Buhari kumpongeza kwa ushindi, na yeye akakubali kushindwa. Kupitia hatua hiyo ya kihistoria katika siasa za Nigeria, Jonathan amewashukuru wanigeria kwa kumpa nafasi ya kuiongoza nchi yao, na kuahidi kuendelea kutoa mchango wake katika masuala ya kitaifa mnamo siku za usoni. ''Nimemtumia General Muhammadu Buhari salamu zangu binafsi za pongezi, na kumtakia kazi njema'', amesema rais Goodluck Jonathan.

Kutimiza ahadi kwa taifa

Goodluck Jonathan, rais wa sasa wa Nigeria ambaye amekubali kushindwa

Goodluck Jonathan, rais wa sasa wa Nigeria ambaye amekubali kushindwa

Goodluck Jonathan amesema aliahidi Nigeria uchaguzi huru na wa haki, na ametimiza ahadi yake. ''Hakuna ndoto yoyote ya kisiasa ambayo inaruhusiwa kusababisha umwagaji wa damu ya wanigeria'', amesema tena Jonathan katika tangazo lake la kukubali kushindwa.

Chama chake cha People's Democratic Party, PDP kimekuwa madarakani nchini Nigeria tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999, lakini ushawishi wake umekuwa ukididimia kutokana na mkururu wa kashfa za ufisadi, na kukithiri kwa mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Miongo mitatu baada ya kuchukua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi, Muhammadu Buhari amekuwa mnigeria wa kwanza kumuangusha rais aliyekuwapo madarakani kwa njia ya uchaguzi.

Katika mji wa Kaduna ulio Kaskazini mwa Nigeria, na ambao wakazi wake ni mchanganyiko wa wakristo na waislamu, wafuasi wa bwana Buhara walijimwaga mitaani, wakipeperusha bendera na kushangiria, baada za mgombea wao kutangazwa mshindi. Katika uchaguzi wa mwaka 2011, watu wasiopungua 800 waliuawa mjini humo katika ghasia za baada ya uchaguzi.

Ukomavu wa kisiasa kwa Nigeria

Kwa wafuasi wa Buhari ilikuwa ni furaha isio na kifani

Kwa wafuasi wa Buhari ilikuwa ni furaha isio na kifani

Hatua ya rais Jonathan ya kukubali hadharani kwamba chama chake kimeshindwa, inatarajiwa kutuliza hasira na machungu ya kushindwa miongoni mwa wafuasi wake.

Msemaji wa chama cha APC cha Muhammadu Buhari, Lai Mohammed amesema walikuwa na wasi wasi kwamba Jonathan asingekubali kushindwa, na kuongeza kuwa hatua yake hiyo itamfanya kuendelea kuwa shujaa.

Umoja wa Ulaya umempongeza Muhammadu Buhari kwa ushindi wake, na kusema unatarajia kufanya kazi naye. Mkuu wa sera za nje wa umoja huo Federica Mogherini amemshukuru pia rais Goodluck Jonathan kwa mchango wake katika kuijenga Nigeria, na kuimarisha demokrasia mnamo miaka mitano iliyopita.

Marekani kwa upande wake imekuwa makini katika kutoa pongezi zake. Afisa wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe, akizungumza wakati ilipokuwa dhahiri kuwa Buhari alikuwa akielekea kwenye ushindi, amesema Marekani itashirikiana na yeyote atakayeibuka mshindi kwa njia ya kidemokrasia.

Amesema Buhari ameshiriki kwa njia ya amani katika chaguzi kadhaa zilizopita, na kamba mara zote alikubali matokeo, hata pale alipokuwa hakubaliani na namna mchakato wa uchaguzi ulivyoendeshwa.

Ushindi wa Muhammadu Buhari umeanzisha ukurasa mpya katika siasa za Nigeria, nchi ambayo tangu kupata uhuru wake kutoka Uingereza miaka 55 iliyopita imeshuhudia mapinduzi ya kijeshi mara sita, na miaka 16 mfululizo ya utawala wa kiraia ulioongozwa na chama cha PDP cha rais Goodluck Jonathan, ambacho mara hii kimekubali kushindwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Hamidou, Oumilkheir

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com