1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit: Umoja wa Ulaya na Uingereza kuendelea na mazungumzo

Zainab Aziz Mhariri: Yusuf Saumu
13 Desemba 2020

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema mazungumzo kati ya Umoja huo na Uingereza yataendelea. Von der Leyen ameeleza kuwa wajumbe wa jumuiya hiyo wamepewa jukumu la kuendelea na mazungumzo.

https://p.dw.com/p/3meYr
Belgien EU Brexit l EU-Kommissionspräsidentin von der Leyen und der Britische Premierminister Johnson
Picha: Olivier Hoslet/AP/picture alliance

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johson alipozungumza na baraza lake la mawaziri ameeleza kwamba ana matumaini ya kufikiwa makubaliano ya kibiashara na Jumuiya ya Ulaya ingawa bado mzungumzo hayo yanakabiliwa na vipengele vigumu. Kwa mara ya kwanza mazungumzo yataendelea bila ya kuweka muda maamlumu. Rais wa Umoja wa Ulaya amesema pande mbili hizo zimeamua kupiga hatua ndefu zaidi katika kufanya mazungumzo ili kuweza kufikia makubaliano.

Wajumbe wakuu kwenye mazungumzo Michel Barnier wa Umoja wa Ulaya na David Frost wa Uingereza wanafanya juhudi za dakika za mwisho ili kufikia makubaliano. Pande hizo mbili zimesema zitaendelea na mazungumzo juu ya biashara huru kuvuka muda wa mwisho wa leo Jumapili 13.12.2020 uliowekwa hapo awali. Rais wa halmashauri wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema litakuwa jambo la busara kupiga hatua ndefu zaidi ili kuweza kufikia lengo la kupatikana makubaliano.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya, Uingereza zarejea kwenye meza ya mazungumzo

Hapo awali wajumbe wakuu kwenye mazungumzo waliendela na mikutano kujadili mkataba juu ya uhusiano wa hapo baadae baina ya Umoja wa Ulaya baada ya Uingereza kujiondoa kwenye jumuiya hiyo mwishoni mwa mwezi huu. Mazungumzo kati ya pande mbili hizo yameshachukua muda wa takriban mwaka mmoja hadi sasa. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kila linalopasa lifanyike ili kuleta makubaliano.

Wajumbe wakuu kwenye mazungumzo ya Brexit. Kushoto David Frost wa Uingereza. Kulia: Michel Barnier wa Umoja wa Ulaya.
Wajumbe wakuu kwenye mazungumzo ya Brexit. Kushoto David Frost wa Uingereza. Kulia: Michel Barnier wa Umoja wa Ulaya.Picha: Oliver Hoslet/REUTERS

Mazungumzo ya leo Jumapili yalikuwa katika jumla ya juhudi za kuondoa vizingiti wakati ambapo kipindi cha mpito kwa Uingereza kinakaribia mwisho. Uingereza ilijiondoa rasmi Umoja wa Ulaya tarehe 31 Desemba mwaka uliopita lakini iliendelea kufuata taratibu kadhaa za Umoja wa Ulaya. Siku ya mwisho ya kufuata taratibu hizo itakuwa hapo tarehe 31 ya mwezi huu.

Mazungumzo yamekwama kutokana hasa na msimamo wa Uingereza wa kushikilia kufanya biashara na Umoja wa Ulaya kwa masharti machache kwa kadri itakavyowezekana. Kwa upande wake Umoja wa Ulaya unaitaka Uingereza ifuate taratibu za jumuiya hiyo ili kuhakikisha ushindani katika msingi wa usawa. Hata hivyo Uingereza inadai kwamba Umoja wa Ulaya unaizuia nchi hiyo kuwa na uhuru wa kupitisha maamuzi yake.

Hofu ya Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya unahofia huenda Uingereza ikateremsha vigezo vya kijamii na vya mazingira sambamba na kuzipa ruzuku kampuni zake kwa kutumia fedha za serikali na hivyo kuipa nchi hiyo fursa kubwa zaidi katika ushindani wa kibiashara. Licha ya rais wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen  kusema kwamba mazungumzo yataendelea, hapo awali waziri wa mambo ya nje  wa Uingereza Dominic Raab alisema safari bado ni ndefu.

Soma zaidi: Uingereza haitabadilisha msimamo kuhusu Brexit

Ikiwa mapatano hayatapatikana Uingereza itakabiliwa na vurumai kutokana muda wa kujitayarisha kuwa mfupi. Bila ya makubaliano na Umoja wa Ulaya Uingereza italazimika kufanya biashara na jumuiya hiyo katika msingi wa sheria za shirika la biashara duniani WTO. Hata hivyo mfumo huo utahusisha kuwekeana ushuru na vizingiti vingine.

Masuala mengine yanayotatiza mazungumzo ni pamoja na mambo ya uvuvi na jinsi ya kusimamia vipengele vya mkataba endapo utafikiwa. Waziri mkuu Boris Johnson amesema Uingereza itasonga mbele uwepo mkataba au bila ya mkataba!

Vyanzo: AP/https://p.dw.com/p/3me2Q