1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit: Theresa May ataka wabunge wampe muda zaidi

Zainab Aziz
10 Februari 2019

Zikiwa zimebaki siku 47 tu kwa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, serikali yawataka wabunge wampe Waziri Mkuu Theresa May muda zaidi wa kurekebisha mpango wake wa kuiondoa nchi hiyo kutoka kwenye Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3D5UP
Brüssel Besuch Theresa May bei Juncker
Picha: Getty Images/D. Mouhtaropoulos

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May anakusudia kuliomba bunge la nchi yake limpe muda zaidi ili aweze kufanya mazungumzo na Umoja wa Ulaya juu ya kuubadilisha mkataba wa Brexit uliopo sasa.

Wiki ijayo bibi May anatarajiwa kutoa taarifa bungeni juu ya hatua aliyofikia kwenye mazungumzo anayofanya na Umoja wa Ulaya. Waziri wa masuala ya jamii, James Borokenshire amesema bunge linatakiwa kupitisha maamuzi kuhusu mpango huo wa May, hadi Februari 27.

Jitihada hiyo inalenga kuepusha mvutano hapo siku ya Alhamisi, wakati bunge litakapo jadili na kuzipigia kura hatua zinazofuata kuhusu mchakato wa Brexit. Baadhi ya wabunge wanataka kufanikisha uwezekano wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya katika msingi wa mkataba.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/F. Lenoir

Uingereza inatakiwa kuondoka Umoja wa Ulaya ifikapo Machi 29 lakini Bunge mwezi uliopita liliukataa mpango wa Brexit wa waziri mkuu huyo hali iliyo mlazimu May kutafuta uwezekano wa kuyafanyia mabadiliko makubaliano yaliyopo sasa na Umoja wa Ulaya ambao umesema hauko tayari. Kikwazo hicho kinaweza kuisababisha Uingereza kuondoka kutoka kwenye Umoja wa Ulaya bila ya mkataba.

May amesema anataka kuuleta tena mpango uliorekebishwa bungeni haraka iwezekanavyo. Ameahidi kuwa, ikiwa hakurudisha mapendekezo yake mapya kwa ajili ya kupigiwa kura ifikapo Februari 13, basi wabunge wataweza kujadili suala la Brexit Februari mnamo tarehe 14 Februari. Vyombo vya habari vya Uingereza vilimeripoti kwamba kura mpya juu ya mpango wa Brexit waTheresa May inaweza kufanyika Februari 25.

Hata hivyo wapinzani wa serikali wanadai kwamba waziri mkuu May anapoteza muda kwa makusudi ambapo bunge litakabiliwa na uchaguzi wa dakika ya mwisho na hivyo wabunge watalazimika kufanya maamuzi kati ya mpango wake au Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya bila ya mkataba.

Mwandishi:Zaianab Aziz/RTRE/AP/DPA
Mhariri: Lilian Mtono