Brazil yaichinja Cameroon, Mexico yaituliza Croatia | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 24.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Brazil yaichinja Cameroon, Mexico yaituliza Croatia

Wenyeji Brazil watakutana na Chile katika hatua ya mchujo baada ya kuigagadua Cameroon magoli 4-1. Neymar alifungua karamu ya magoli ya Brazil katika dakika ya 17akiweka kimyani goli lake la nne la mashindano haya.

Mchezaji Joel Matip aliipatia Cameroon goli la kusawazisha na la kwanza katika mashindano ya mwaka, huu chini ya dakika 10 baadaye, akifunga kwa mpira wa Allan Nyom, ambaye alitumia vyema makosa ya mlinzi Dani Alves kushoto mwa boxi la Brazil.

Neymar alifunga bao lake la pili la mchezo huo na la nne katika mechi tatu, na kuipa Brazil uongozi wa mabao 2-1 dakika kumi kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika. Fred aliifungia Brazil goli la tatu mwanzoni mwa kipindi cha pili, na mchezaji wa akiba Fernandinho alihitimisha na la nne dakika tano kabla ya firimbi ya mwisho.

Fußball WM 2014 Brasilien - Kamerun

Cameroon walijaribu Kila mbinu kuwakosesha furaha wenyeji Brazil, lakini mbinu zao ziliambulia patupu

Ushindi huo ulikuwa ni ahueni kwa wenyeji hao baada ya mwanzo wa mashindano usiyoridhisha kutilia mashaka hadhi yao kama moja ya timu zinazopewa nafasi ya kubeba kombe la mwaka huu. Ushindi huo umewaacha katika uongozi wa kundi A, mbele ya Mexico ambayo iliwabana mbavu kwa sare tasa. Hivyo basi Brazil watakuana na Chile katika mechi ya mchujo

Mexico yaiangamiza Croatia

Mexico ilijihakikishia nafasi katika raundi ya pili ya mashindano ya kombe la dunia kwa mara ya sita mfululizo kwa kushindilia Croatia magoli 3-1. Rafael Marquez, Andre Guadado na Javier "Chicharito" Hernandez wote walifunga katika muda wa dakika 10 na kuiangamiza timu yenye vipaji ya Croatia kwenye hatua ya makundi.

Fußball WM 2014 Kroatien Mexiko

Beki mkongwe Marquez alionyesha kuwa anaweza bado kuruka juu zaidi na kuwahangaisha Wacroatia

Wacroatia walitakiwa kushinda ili kuweza kusonga mbele, na walimiliki mpira kwa sehemu kubwa, lakini walipata tabu kuliona lango la Guillermo Ochoa, ambaye alizuwia juhudi zao zote hadi goli la kufutia machozi la dakika ya 87 lililofungwa na Ivan Perisic.

Mexico waliingia katika mchezo wa jana wakihitaji tu sare na walionekana kuwa wa hatari katika mashambulizi, lakini Croatia iliwamudu hadi mpasuko wa magoli matatu. Alikuwa Marques alieshambulia kwanza, akimpiga chenga mlinzi wa Croatia Vedran Corluka na kuweka kimyani mpira wa kona iliyopigwa na Hector Herrera katika dakika ya 72.

Dakika tatu baadaye, Guardado alizitikisa nyavu kwa mkwaju mzito kufuatia krosi kutoka kwa Oribe Peralta. Na baadaye katika ya 82, mchezaji maarufu wa Manchester United Hernandez, ambaye amekuwa mchezaji wa akiba wa kipindi cha pili katika mechi zote tatu za Mexico, alifunga kwa kichwa kufuatia kona ya Herrera.

Mexico sasa watacheza dhidi ya Uholanzi, ambao walimalizia usukani mwa kundi B, baada ya kuishinda Chile kwa magoli 2-0 katika mchezo uliyotangulia.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com